Orbán na Xi Jinping wajadili mzozo wa Ukraine na Urusi
9 Julai 2024Majadiliano hayo yamefanyika baada ya Orbán kufanya ziara ya ghafla mjini Beijing, muda mfupi baada ya kuzungumza na Rais wa Urusi Vladmir Putin.
Orbán amefanya ziara hiyo ya kushtukiza China wakati huu nchi yake ikiwa mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya. Kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X, ametaja sababu ya kufanya ziara hiyo akisema kuwa China ni taifa muhimu katika kutengeneza mazingira ya amani kwenye mzozo wa Urusi na Ukraine.
Soma zaidi: Xi ataka Urusi na Ukraine kusaidiwa kuwa na mazungumzo ya amani
Ameipongeza pia nchi hiyo kwa juhudi zake muhimu za amani alizoziita kuwa ni muhimu na zenye kujenga. Zaidi Rais Xi Jinping alimueleza Orbán kuwa, mataifa yenye nguvu duniani yanapaswa kuzisaidia Urusi na Ukraine ziweze kuanza mazungumzo ya kutafuta amani. China imekuwa ikipigia debe mpango wake wa amani kwenye mzozo huo wenye vipengele sita, uliotolewa sambamba na Brazil mnamo mwezi Mei.
Beijing imekuwa ikijipambanua kuwa isiyoegemea upande wowote katika mzozo huo. Ziara ya Orbánnchini China imefanyika wakati Jumuiya ya kujihami ya NATOikifanya mkutano wake wa kilele kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwake. Sehemu kubwa ya mijadala ya mkutano huo inatajwa kuwa changamoto zinazoikabili Ukraine.
Marekani yaonesha wasiwasi baada ya mazungumzo ya Orbán na Jinping
Katika hatua nyingine Marekani imeelezea wasiwasi wake baada ya kukutana kwa viongozi hao wa Hungary na China. Msemaji wa baraza la usalama wa taifa wa Marekani John Kirby amsema kuwa ziara ya Orbán nchini China haionekani kuwa yenye manufaa katika suala la kuisaidia Ukraine
Viktor Orbán amekuwa akipinga waziwazi misaada ya mataifa ya magharibi kwa Ukraine. Kiongozi huyo amekuwa akizuia au kuchelewesha juhudi za Umoja wa Ulaya za kuisaidia Kyiv na kuiwekea vikwazo Urusi kutokana na uvamizi wake.