1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia yakosolewa kuhusu wahamiaji

20 Julai 2018

Askari wa kikosi cha ulinzi wa pwani nchini Italia wamelalamika juu ya uamuzi wa serikali mpya ya Italia wa kuwazuia wahamiaji wanaookolewa baharini kwa kuzifunga bandari zake, wakisema hatua hiyo inasababisha taharuki.

https://p.dw.com/p/31oIG
Mittelmeer Lesbos Bootsflüchtlinge
Picha: picture-alliance/NurPhoto/M. Heine

Askari wa kikosi cha ulinzi wa pwani nchini Italia wamelalamika juu ya uamuzi wa serikali mpya ya Italia wa kuwazuia wahamiaji wanaookolewa baharini kwa kuzifunga bandari zake, wakisema hatua hiyo inasababisha taharuki kwa jeshi hilo, ambalo hadi sasa limetoa mchango mkubwa katika operesheni za kuwaokoa wahamiaji hao. 

Kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita walinzi wa pwania wamekuwa wakiratibu shughuli ya uokozi wa mamia kwa maelfu ya wahamiaji karibu na pwani ya Libya, na katika matukio mengi huwaokoa majini wakiwa katika hali mbaya.

Lakini kuanzia mwezi Juni, walipewa amri ya kuhamishia mawasiliano ya simu za kuomba msaada na ripoti za boti zinazokumbwa na matatizo baharini mjini Tripoli, Libya.

Hivi sasa baadhi ya wafanyakazi hao wameikosoa serikali hadharani, licha ya kwamba kitamaduni, haikubaliki kuikosoa serikali.

Kwenye mahojiano na gazeti la kila siku la Italia, la 11 Sole 24 Ore, mnamo wiki iliyopita, kamanda wa ngazi za juu wa kikosi cha ulinzi wa pwani amekosoa msimamo mpya mkali wa serikali ya Italia na hususan, wa waziri wa mambo ya ndani mwenye siasa kali za mrengo wa kulia Matteo Salvin.

Alipozungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, kamanda huyo alikumbushia kwamba mfumo wa kisheria wa Italia uliichukulia Libya kama sio mahali salama kwa ajili ya wahamiaji waliookolewa kurejeshwa huko.

Itanlien Minister Salvini
Waziri wa mambo ya ndani wa Italia, Matteo Salvini anatuhumiwa sana kwa misimamo yake mikali kuhusu wahamiaji.Picha: Reuters/T. Gentile

UN yapongeza mataifa ya Ulaya kwa kukubaliana kuhusu wahamiaji waliokwama Mediterania

Wahamiaji wengi wanaojaribu kwenda Ulaya huwa hawapo tayari kurejea Libya, kwa kuwa hukabiliwa na manyanyaso na kubakwa wakiwa kwenye vituo vya kuwashikilia wahamiaji.

Kamanda huyo, pia amelaani hatua ya kukosekana na amri rasmi ama kuchukua hatua kwa kuangazia maamuzi ya kuzizuia meli zilizobeba wahamiaji kutia nanga kwenye bandari za nchini humo.

Lakini katika hatua nyingine, naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari hii leo, katika makao makuu ya Umoja huo, yaliyoko New York Marekani kwamba shirika la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limekaribisha hatua za hivi karibuni za baadhi ya nchi za Ulaya za kuungana pamoja kumaliza mvutano juu ya wakimbizi na wahamiaji 450 waliokwama katika bahari ya Mediterania, wakati kukiwa na mvutano kuhusu meli yao inakoweza kutia nanga.

Libya kupitia waziri wake mkuu Fayez al-Sarraj imesema haitaruhusu Umoja wa Ulaya kujenga vituo vyake vya kuchunguza maombi ya waomba hifadhi nchini mwake, hatua inayochukuliwa kama pigo jipya kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaosaka suluhu ya kukabiliana na wahamiaji wapya wanaoingia Ulaya.

Saraj, amesema hayo katika mahojiano na gazeti la kila siku la Ujerumani la Bild, na kuongeza kuwa hawataafiki makubaliano yoyote na Umoja wa Ulaya, ya kuwataka kuwapokea wahamiaji haramu, na kusema viongozi hao wa Ulaya badala yake wanatakiwa kuongeza shinikizo kwa mataifa wanakotokea wahamiaji kuwazuia kuondoka.

Morocco na Albania, zenyewe zimekwishaeleza wazi kutokukubaliana na mpango huo wa Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE

Mhariri:Iddi Ssessanga