Israel yafanya mashambulizi Palestina, Syria na Lebanon
13 Septemba 2024Duru za kuaminika zinazofuatilia vita hivyo zimeeleza hivi leo kuwa siku chache zilizopita, vikosi vya Israel vilisafiri kwa helikopta hadi nchini Syria na kufanya mashambulizi yaliyoharibu kituo kinachofahamika kama Hair Abbas chenye handaki la kutengenezea makombora lililojengwa chini ya usimamizi wa Iran. Kituo tofauti cha utafiti wa kisayansi kinachojihusisha na uzalishaji wa silaha kiliharibiwa pia.
Hata hivyo jeshi la Israel ambalo limefanya mamia ya mashambulizi nchini Syria tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2011, lilikataa awali kuzungumzia operesheni hiyo ilianza siku ya Jumapili lakini baadaye ikathibitisha na kusema walifanikiwa kuwaua "magaidi" ambao wamekuwa wakiishambulia Israel.
Soma pia: Iran yapongeza shambulizi la Hezbollah dhidi ya Israel
Mamlaka ya Syria ilisema watu 18 waliuawa katika mashambulizi ya Israel kwenye "maeneo ya kijeshi" huko Masyaf mkoani Hama, huku shirika la kuchunguza vita na haki za binaadamu la Syria likiripoti vifo vya watu 27.
Syria na Iran ziliitupia Israel lawama kutokana na uvamizi huo, huku Tehran ikitaja kuwa ni "shambulio la jinai". Mbali na mashambulizi hayo nchini Syria, Israel imekuwa ikikabiliana karibu kila siku na kundi la wanamgambo la Hezbollah la Lebanon. Leo hii mamia ya watu walihudhuria mazishi ya watu wawili waliouawa nchini Lebanon. Sheikh Ahmed Murad, ni afisa wa Hezbollah:
"Adui huyu mwoga hulenga vijana wasio na hatia na wale ambao ni fahari ya familia zao. Kosa lao pekee ni kuwa wenyeji wa eneo hili la milima na kuwa miongoni mwa wapinzani. Upinzani utajibu shambulizi hili baya. Utalipiza kisasi kwa watu wasio na hatia iwe watoto, kaka na baba zetu na kila mtu ambaye aliuawa kwa njia isiyo ya haki na adui huyu mbaya anayefanya uhalifu wake huko Lebanon, Palestina, Syria na ukanda wote huu."
Hamas yaishukuru Hezbollah kwa uungwaji mkono katika vita vyake na Israel
Kiongozi mkuu wa Hamas Yahya Sinwar amemshukuru kiongozi wa Hezbollah Sayyed Hassan Nasrallah kwa uungwaji wake mkono katika mzozo na Israel, ukiwa ni ujumbe wa kwanza kuripotiwa tangu Sinwar alipochukua uongozi wa Hamas mwezi Agosti baada ya mauaji ya Ismail Haniyeh mjini Tehran.
Soma pia: Volker Turk azitaka nchi kuchukua hatua dhidi ya Israel
Katika tukio jingine, Ubalozi wa Marekani nchini Iraq umeyalaani leo Ijumaa makundi yenye mafungamano na Iran kufuatia shambulio la wiki hii kwenye ofisi ndogo ya Marekani katika uwanja wa ndege wa Baghdad, na kuonya kuwa bado Washington ina haki ya kujilinda.
Shambulio hilo lilitokea huku kukiwa hali ya mvutano wa kikanda kuhusu vita vya Gaza na muda mfupi tu kabla ya ziara ya Rais wa Iran Masoud Pezeshkian nchini Iraq. Matukio yote hayo yamekuwa yakiongeza hofu ya kuzuka kwa vita vipana zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Vyanzo: (DPAE, AP, RTRE, AFP)