1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran yapongeza shambulizi la Hezbollah dhidi ya Israel

26 Agosti 2024

Iran imepongeza shambulizi la droni na makombora lililofanywa na kundi la Hezbollah nchini Lebanon dhidi ya Israel, ikisema adui yake mkuu amepoteza uwezo wa kuzuia mashambulizi kama hayo.

https://p.dw.com/p/4jwGP
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kanani akihutubia waandishi habari mnamo Februari 19,2024
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser KananiPicha: Rouzbeh Fouladi/ZUMA Press Wire/picture alliance

Katika ujumbe aliochapisha katika mtandao wa kijamii wa X, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kanani, amesema utawala wa Kizayuni hautaweza kuwa na uwezo wa kuficha, kupotosha au kuhakiki baadhi ya ukweli kuhusu operesheni ya kundi la Hezbollah lakini unajua vyema kwamba ukweli uliopo hautabadilika.

Kanani asema jeshi la Israel limepoteza uwezo wa kushambulia 

Kanani ameongeza kusema jeshi la Israel limepoteza uwezo wake wa kushambulia na kuzuia mashambulizi na sasa lazima ijilinde dhidi ya mashambulizi ya kimkakati.

Pia aliikosoa Marekani kwa kuiunga mkonoIsrael ambayo imeshindwa kutabiri wakati na mahali pa vitendo vya Hezbollah.

Soma pia:Hamas yakataa matakwa mapya ya Israel usitishaji vita vya Gaza

Siku ya Jumapili, spika wa bunge la Iran Mohammad Bagher Ghalibaf, alifananisha shambulizi hilo na kushindwa kwa jeshi la Israel katika vita vyake na Hezbollah mnamo mwaka 2006.

Wagonjwa waanza kukimbia hospitali ya Al-Aqsa huko Deir al-Balah

Jeshi la Israel limesema halijaagiza kuondoka kwa watu kutoka hospitali ya Al-Aqsa huko Deir al-Balah, inayohudumu katika eneo la Kati mwa Gaza, lakini wagonjwa na watu waliopata hifadhi katika eneo hilo wanahofia kwamba huenda ikakumbwa na mapigano au kuwa shabaha ya uvamizi wa Israel.

Shirika la habari la Associated Press, limeripoti kuona watu wakikimbia hospitali hiyo na maeneo jirani hii leo, wengi wao kwa miguu. Watu pia wamekimbia kutoka shule nne katika eneo hilo.

Wapalestina waliopoteza makazi yao kutokana na shambulizi la anga la Israel katika ukanda wa Gaza wakitembea katika barabara za mji wa kusini wa Khan Younis huko Gaza mnamo Julai 4,2024
Wapalestina waliopoteza makazi yao kutokana na shambulizi la anga la Israel katika ukanda wa GazaPicha: Jehad Alshrafi/AP/picture alliance

Hospitali hiyo inasema ilikuwa ikiwatibu zaidi ya wagonjwa 600 kabla ya maagizo ya kuhamishwa yaliyotolewa kwa maeneo ya makaazi yalioko umbali wa kilomita moja.

Katika ujumbe kwenye ukurasa wa X, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, MSF, limesema mripuko uliotokea umbali wa mita 250 kutoka hospitali hiyo hapo jana, ulisababisha hofu, na kuchangia kasi ya kuondoka kwa watu.

MSF yazingatia kudumisha matibabu ya kuokoa maisha

Kutokana na hali hiyo, MSF inazingatia iwapo isitishe huduma ya kushughulikia majeraha kwasasa, huku ikijaribu kudumisha matibabu ya kuokoa maisha.

Misri haijakubali uwepo wa Israel katika kivuuko cha mpaka cha Rafah 

Misri imesisitiza kwamba haijakubali uwepo wa Israel katika kivuuko cha mpaka cha Rafah ama uchochoro wa Philadelphi. Haya ni kulingana na kituo cha habari cha  Al Qahera kinachohusishwa na serikali, kilichonukuu chanzo kimoja kikuu.

Suala moja kuu katika mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza limekuwa msisitizo wa Israeli juu ya uwepo wake katika ukanda huo wa Philadelphi wa kilomita 14.5 katika mpaka wa Kusini kati ya Gaza na Misri.