Iran yalaaniwa vikali katika kura ya Baraza la Usalama
12 Januari 2024Katika azimio hilo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limeilaani Iran ambayo ni muuzaji mkuu wa silaha kwa WaHouthi. Azimio hilo lililowasilishwa kwenye baraza la usalama na Marekani na Japan liliidhinishwa kwa kura 11. Nchi nne Urusi, China, Algeria na Msumbiji hazikupiga kura.
Azimio hilo limelaani "kwa maneno makali" mashambulizi yanayofanywa na Wahouthi ya kuzilenga meli za biashara, ambazo limesema kuwa mashambulizi hayo yanazuia biashara ya kimataifa na pia yanadhoofisha uhuru wa kuendesha shughuli za vyombo vya baharini.
Soma Pia: Vikosi vya Marekani na Uingereza vyatungua droni na makomba ya Wahouthi
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield kabla ya zoezi la kupiga kura alisema azimio walilowasilisha linadai kwamba WaHouthi wasitishe mashambulizi yao ya kinyama na yanayokiuka sheria za kimataifa. Amesema azimio hilo linafuata hatua za Baraza la Usalama zinazosisitiza haki za utendaji na uhuru wa vyombo vya baharini vya maeneo yote katika Bahari ya Shamu, haki hizo zinajumuisha wafanyabiashara na meli za kibiashara zinazopitia kwenye njia ya Bab-el-Mandeb kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield amesema msisitizo huo wa Umoja wa Mataifa unaonyesha wazi kwamba shughuli za kibiashara kwa njia za meli katika Bahari ya Sham hazipaswi kuzuiwa.
Akizungumza baada ya kumalizika zoezi la kupiga kura, Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vasily Nebenzya amesema, nchi yake inasisitiza tena kwamba Azimio lililopitishwa lisiwe ni hatua ya kuhalalisha mashambulizi katika Bahari Shamu ya muungano unaoitwa (Operesheni Mafanikio) wa kujibu mashambulizi ya Wahouthi ulioundwa na Marekani na washirika wake. Na amekumbusha kuwa operesheni hiyo inapaswa kufanywa kwa kuzingatia sheria zilizopo za kimataifa.
Marekebisho matatu kwenye azimio hilo yaliyopendekezwa na Urusi pia yalipigiwa kura lakini hakuna hata moja lililofanikiwa kupita.
Waasi wa Houthi, ambao wamekuwa vitani dhidi ya serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa tangu mwaka 2014, wamesema walianzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kukomesha mashambulizi mabaya ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, na wamelipuuza azimio hilo wakilitaja kuwa ni mchezo wa kisiasa, huku wakiishtumu Marekani kuwa ndiyo inavunja sheria za kimataifa.
Vyanzo: DPA/AP