Marekani yazindua muungano wa ulinzi wa Bahari ya Shamu
19 Desemba 2023Austin, ambaye yuko ziarani Bahrain, makao makuu ya jeshi la wanamaji la Marekani katika Mashariki ya Kati, amesema Uingereza, Bahrain, Canada, Ufaransa, Italia, Uholanzi, Norway, Ushelisheli na Uhispania, ni miongoni mwa mataifa yanayohusika katika operesheni hiyo ya usalama wa Bahari ya Shamu.
Soma pia:Wahouthi wazishambulia meli za Marekani kwa droni
Ufaransa ilisema baadaye kwamba itajiunga na juhudi hizo za kulikomesha kundi hilo la waasi.
Muungano unafanya doria za pamoja
Muungano huo, utafanya doria za pamoja katika eneo la Kusini mwa Bahari hiyo ya Shamu katika Ghuba ya Aden.
Katika taarifa, Austin amesema kwamba hii ni changamoto ya kimataifa inayohitaji hatua ya pamoja na kuutangaza muungano huo kama Msimamizi wa Operesheni ya Ufanisi.
Austin atoa wito kwa mataifa kuchangia katika juhudi za kulinda Bahari ya Shamu.
Soma pia:Waasi wa Yemen watishia kushambulia meli zinazoelekea Israel kutokea bahari ya shamu
Katika mkutano uliofanywa kwa njia ya video na mawaziri kutoka mataifa zaidi ya 40, Austin alitoa wito kwa nchi zingine kuchangia huku akilaani vitendo hivyo vya kundi hilo la Wahouthi.
Tangazo la Austin hata hivyo linaacha maswali mengi, ikiwa ni pamoja na mataifa mangapi yako tayari kufanya kile ambacho meli nyingi za kivita za Marekani zimefanya katika siku za hivi karibuni, kudungua makombora na ndege zisozo na rubani za Wahouthina kutoa msaada kwa meli za kibiashara zinazoshambuliwa.
Baadhi ya makampuni yabadilisha njia ya safari zao
Kampuni za usafirishaji ziliendelea kugeuza njia ya safari zao baharini licha ya tangazo la Austin.
Kampuni ya Maersk ya Denmark, ambayo ilikuwa imesimamisha safari zake kupitia Bahari ya Shamu, imesema itapeleka meli zake kuzunguka kupitia Afrika hadi itakapotangaza tena.
Soma pia:Meli ya kivita ya Marekani yazuia mashambulizi ya Wahouthi
Meli nyingine nyingi bado zilikuwa zinapitia njia hiyo ya bahari. Meli kadhaa zinazotumia Bahari ya Shamu zimebeba walinzi wenye silaha.
Vyanzo vya sekta hiyo ya usafirishaji vinasema athari kwa biashara ya kimataifa itategemea muda ambao mgogoro huo utachukuwa lakini malipo ya bima na njia ndefu zitakuwa changamoto za sasa hivi.
Waasi wa Houthi wasema hawatazuiwa na muungano huo mpya
Waasi wa Houthi, ambao wanadhibiti maeneo makubwa ya Yemen, wametishia kulenga meli zote zinazoelekea Israel, bila kujali utaifa wao, na kuonya makampuni ya kimataifa dhidi ya kujishughulisha na bandari za Israeli. .
Kundi hilo limesema leo kuwa muungano huo unaoongozwa na Marekani hautawazuia.