Iran yaidhinisha wagombea sita wa uchaguzi wa urais Juni 28
9 Juni 2024Wagombea hao waliotangazwa na wizara ya mambo ya ndani walichaguliwa kutoka orodha ya watu 80 waliosajiliwa na Baraza la Uongozi lenye ushawishi mkubwa linalosimamia uchaguzi katika jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Miongoni mwa walioidhinishwa ni spika wa bunge mhafidhina Mohammad Bagher Ghalibaf na mjumbe wa zamani wa mazungumzo ya nyuklia mwenye msimamo mkali wa kihafidhina Saeed Jalili.
Ni mgombea mmoja tu mwanamageuzi, Massoud Pezeshkian, ambaye ni mbunge anayewakilisha jimbo la Tabriz katika bunge la Iran, aliyeidhinishwa.
Soma pia: Mshirika wa Khamenei ajisajili kuwania urais Iran
Waziri wa zamani wa mambo ya ndani mhafidhina Mostafa Pourmohammadi pia ameruhusiwa kugombea.
Rais wa zamani mwenye msimamo mkali Mahmoud Ahmadinejad, ambaye alifungiwa kushiriki mbio za urais katika mwaka mwaka wa 2017 na 2021, tena ametupwa nje kwenye orodha hiyo.
Wengine kwenye orodha hiyo ni meya wa Tehran mhafidhina Alireza Zakaani na makamu wa rais wa sasa Amirhossein Ghazizadeh-Hashemi, ambaye ni mhafidhina wa msimamo mkali anayeongoza Wakfu wa Mashahidi.
Katika uchaguzi wa mwaka wa 2021, Baraza la uongozi liliwaondoa kwenye orodha wagombea kadhaa wanamageuzi na wa siasa za wastani kabla ya uchaguzi wa rais ambao ulimuweka madarakani kiongozi aliyekuwa wa msimamo mkali wa kifadhina, Raisi.