Spika wa zamani wa bunge la Iran kuwania urais
31 Mei 2024Larijani amewasilisha nia yake ya kuwania urais katika kura ya ghafla iliyoitishwa baada ya kifo cha rais wa nchi hiyo Ebrahim Raisi aliyefariki dunia katika ajali ya helikopta tarehe 19 mwezi huu wa Mei.
Larijani, mtaalamu wa Hisabati mwenye umri wa miaka 66, aliwasilisha ombi lake kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani leo hii Ijumaa. Larijani ameshika nyadhifa kadhaa za uongozi katika miaka ya hivi karibuni, miongoni mwao ni waziri wa utamaduni.
Wachambuzi wanasema Larijani ana uzoefu mkubwa wa kutatua migogoro na hasa katika kuanzisha upya mazungumzo ya nyuklia na nchi za Magharibi.
Mkataba mpya wa nyuklia ndio njia pekee ya kuondoa vikwazo vya kimataifa vilivyowekwa dhidi ya Iran ambapo akifanikiwa ataweza kuumaliza mgogoro mkubwa wa kiuchumi wa miaka mitano unaoikabili nchi hiyo.