Iran yaashiria haina mpango wa kujibu shambulizi la Israel
20 Aprili 2024Afisa huyo ambaye jina lake halikutajwa, amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kilichotekea ni hujuma za kujipenyeza kuliko kuwa mashambulizi yanayoripotiwa na vyanzo vya kigeni.
Hata waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amirabdollahian, akizungumza na wajumbe wa mataifa ya Kiislamu mjini New York, amesema mashambulizi yalifanywa na dronindogo na hayakusababisha uharibifu wowote.
Israel haijatoa taarifa yoyote juu ya mashambulizi hayo inayoripotiwa kuyafanya, na mshirika wake mkuu, Marekani imekataa kujihusisha.
Soma pia:Iran na Israel zatolewa miito ya kutotanua mzozo wa katika eneo la Mashariki ya Kati
Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amefanya mazunguzo na mwenzake wa Israel, lakini taarifa kutoka mazungumzo yao imesema kuwa wamejadili masuala ya kupunguza mivutano, bila kuitaja Iran.
Israel yasema imeruhusu msaada zaidi kuingia Gaza
Israel imearifu jana Ijumaa kuwa imeongeza juhudi za kuingiza misaada ya kiutu kwa wakaazi wa Gaza. Malori 276 yaliyobeba chakula na dawa yaliingia katika Ukanda wa Gaza siku ya Alhamisi, ikiwa ni kwa mujibu wa mamlaka inayohusika na mawasiliano na Wapalestina, COGAT.
Aidha, paleti 144 za chakula zilidondoshwa kutokea angani, na malori mengine 700 yanasubiri nyuma ya kituo cha ukaguzi cha Kerem Shalom, tayari kuchukuliwa na mashirika ya msaada ya Umoja wa Mataifa ya kusambaza chakula.
Kutokana na janga la kibinadamu linalowatishia watu wa Gaza, Israel imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka washirika wake wa magharibi na Umoja wa Mataifa, kuitaka iruhusu haraka kuingizwa kwa shehena zaidi za msaada.
Soma pia:Israel yaendeleza mashambulizi katika ukanda wa Gaza
Ingawa mashirika ya wahisani yametambua ongezeko la msaada unaoingia Gaza, yanasisitiza kuwa bado malori yanayoruhusiwa kuingia hayatoshi, na kulalamika kuwa mapigano yanayoendelea yanakwamisha usambazaji wa msaada unaowasilishwa.