Iran na Israel zatakiwa kutotanua mzozo wao
19 Aprili 2024Katika mkutano wa kundi la nchi saba tajiri zaidi kiviwanda G7 uliokamilika visiwani Capri nchini Italia, Marekani imesema ilipokea taarifa za "dakika za mwisho" kutoka Israel kuhusu hatua yake ya kufanya mashambulizi ya droni nchini Iran, lakini ikasisitiza kwamba haikushiriki katika shambulio hilo.
Mapema leo, Iran ilifyetua makombora kutoka kwenye mfumo wake wa ulinzi wa anga karibu na mji wa Isfahan na kusema wamedungua droni tatu. Hii ilikuwa ni sehemu ya shambulio la Israel la kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi ya Iran mwishoni mwa jumaa lililopita. Hata hivyo serikali mjini Tehran imesema shambulio hilo halikuwa na madhara yoyote na hivyo kwa sasa hawana mpango wowote wa kujibu mapigo.
Katika taarifa ya pamoja baada ya mkutano wa siku tatu, mawaziri wa Mambo ya Nje wa G7 inayozijumuisha Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Marekani wamehimiza pande zote kujizuia na hatua zozote zinazoweza kuuchochea mzozo huo. Akishiriki mkutano huo wa G7, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema:
"Kutokana na taarifa za mashambulizi ya leo, tunatoa wito kwa pande zote kuchukua hatua za kuzuia kuongezeka kwa hali ya mzozo. Na sisi kama G7, tunalifanyia kazi hilo. Kila upande lazima uchukue hatua zenye busara na kuwajibika. Kwa sababu si watu wa Israel wala Iran au katika nchi zingine katika kanda hiyo wanaotaka kutumbukizwa katika janga."
Ukanda wa Mashariki ya Kati mashakani
Wito kama huo umetolewa pia na mataifa mengine kama Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia msemaji wake Stephane Dujarric amesema sasa ni wakati muafaka wa kukomesha muendelezo hatari wa vitendo vya kulipiziana kisasi huko Mashariki ya Kati, huku akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushirikiana ili kuzuia hatua zozote zinazoweza kusababisha janga katika eneo hilo na kwengineko duniani.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan amezungumza leo kwa njia ya simu na mwenzake wa Iran Hossein Amirabdollahian ili kujadili hali inayoendelea katika kanda hiyo. Wakati huo huo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatazamiwa kukutana hii leo na Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati na Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo Joseph Aoun ili kujadili hatua zinazoweza kurejesha hali ya utulivu huko Mashariki ya Kati.
Tarifa za Israel kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Iran, zilipelekea bei ya mafuta kupanda kwa muda mfupi huku masoko ya hisa yakipungua na hivyo kushuhudia masoko yakielekeza zaidi uwekezaji wao kwa bidhaa salama zaidi kama vile dhahabu.
(Vyanzo: Mashirika)