Iran: "Tunayo haki kisheria" ya kuiadhibu Israel
5 Agosti 2024Serikali ya Iran imeapa kuwa italipiza kisasi mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Hanniyeh aliyeuawa wiki iliyopita mjini Tehran. Licha ya Israel kujizuia kuzungumzia tukio hilo, inashutumiwa na Tehran kuhusika na mauaji hayo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Nasser Kanani amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran kuwa Iran haina nia ya kulitumbukiza eneo la Mashariki ya Kati kwenye vita kamili, lakini wanapozungumzia kuhusu haki yao ya kuiadhibu Israel, hii ni hatua ya kusaidia kuimarisha usalama na utulivu katika eneo hilo :
"Tunaamini kuwa uimarishwaji wa usalama ulio thabiti katika eneo hili, utafikiwa kwa kumuadhibu mvamizi huyo na kuweka kizuizi dhidi ya tabia yake ya uhasama na vitisho vya utawala wa Kizayuni hadi nje ya mipaka yake."
Soma pia: Israel yasema haitojizuia ikiwa Iran itaishambulia
Hofu imekuwa ikiongezeka ya kushuhudia eneo zima la Mashariki ya Kati likitumbukia kwenye vita kamili. Mataifa kadhaa yamewataka raia wake kuondoka na kutosafiri kuelekea Lebanon. Wanadiplomasia ya kimataifa wamekuwa wakiendeleza pia juhudi za kupunguza hali ya mvutano.
Sergei Shoigu wa Urusi afanya ziara nchini Iran
Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa la Urusi amewasili hii leo mjini Tehran, huku kukiwa na hofu ya vita vikubwa katika eneo hilo. Sergei Shoigu, waziri wa zamani wa ulinzi wa Urusi, anatazamiwa kukutana na maafisa wakuu wa kijeshi na kiusalama pamoja na kufanya pia mazungumzo na Rais mpya Masoud Pezeshkian ili kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali zikiwemo za usalama.
Urusi ambayo ni mshirika wa Iran ililaani vikali mauaji ya Hanniyeh na sasa ziara hii ya Shoigu inaweza kutafsiriwa kama ishara ya uungwaji mkono kwa Iran wakati ambapo Marekani imesema mara kadhaa kuwa iko tayari kuilinda Israel na vitisho vyote kutoka Iran. Rais Pezeshkian wa Iran ameielezea Urusi kama "mshirika wa kimkakati anayethaminiwa".
Katika hatua nyingine, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya Haki za Kibinadamu Volker Turk ametowa wito leo hii wa kutaka kusitishwa haraka kwa hali ya mvutano huko Mashariki ya Kati kutokana na hofu kwamba vita vya Gaza vinaweza kutanuka zaidi.
Soma pia: Iran na washirika wajadili kisasi cha mauaji ya Haniyeh
Turk ameyataka mataifa yenye ushawishi kuchukua hatua za haraka ili kukomesha hali ambayo amesema sasa imekuwa hatari na kusema katika kipindi cha miezi 10 iliyopita, raia wengi wakiwemo wanawake na watoto, wamepitia madhila na mateso yasiyovumilika kutokana na vita vinavyoendelea huko Mashariki ya Kati.
(Vyanzo: AFP, AP,Reuters)