Israel yasema haitojizuia ikiwa Iran itaishambulia
3 Agosti 2024Afisa huyo amesisitiza kuwa Israel haitojizuia ikiwa Iran itaanzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi kufuatia mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh aliyezikwa jana mjini Doha, Qatar.
Tzachi Hanegbi, mshauri wa usalama wa Israel amelinganisha mvutano wa sasa na ule wa mwezi Aprili, ambapo Iran iliilenga Israel kwa mashambulizi makubwa ya droni zipatazo 330 na makombora ya masafa marefu.
Soma pia: Biden ahofia kusambaa kwa machafuko ya Mashariki ya Kati
Wakati huo Israel ilijizuia kujibu mashambulizi hayo kwa kuheshimu miito ya washirika wake ikiwemo Marekani.
Hanegbi amesisitiza kwamba kwa sasa hali ni tofauti na kuwa Israel ilijizuia mara moja na haitoweza kufanya hivyo mara mbili huku akisisitiza kuwa yeyote atakayeishambulia Israel atalipia gharama kubwa.
Hofu imekua ikiongezeka kuhusu hatari ya kutanuka kwa mzozo huo na kulitumbukiza eneo zima la Mashariki ya Kati katika vita vya kikanda.
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei aliapa kulipiza kisasi kufuatia mauaji ya Hanniyeh katika ardhi yake. Wiki hii Marekani iliihakikishia Israel kwamba itaisaidia kulinda usalama wake na kukabiliana na vitisho vyote kutoka kwa Iran.
(Vyanzo: Mashirika)