1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya wanyama pori ulimwenguni kote yapungua kwa 69%

13 Oktoba 2022

Ripoti ya Mfuko wa Wanyamapori Ulimwenguni (WWF) imesema idadi ya wanyama pori ulimwenguni kote imepungua kwa theluthi mbili tangu mwaka 1970.

https://p.dw.com/p/4I7nZ
Kenia die Dürre hat eine verheerende Wirkung auf die wilden Tiere
Picha: Ed Ram/Getty Images

Kulingana na utafiti uliofanywa, hayo yamesababishwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa misitu na uchafuzi wa bahari.

Ripoti hiyo iliyotolewa Alhamisi na Mfuko wa Wanyamapori Ulimwenguni (WWF) imesema utafiti ulibaini kuwa kwa wastani, idadi ya wanyama pori imepungua kwa asilimia 69.

Wanyamapori wasafirishwa kikatili kutoka Afrika

Utafiti huo ulitumia data ya mwaka 2018  kutoka Chama cha Hifadhi ya Wanyama cha London (ZSL) kuhusu hali ya wanyama 32,000 wa zaidi ya aina 5,000.

Mizoga ya pomboo au dolphin wengi yaopolewa baharini katika kisiwa cha Faeroe Septemba 12, 2021.
Mizoga ya pomboo au dolphin wengi yaopolewa baharini katika kisiwa cha Faeroe Septemba 12, 2021.Picha: Sea Shepherd/AP/picture alliance

Maeneo ya Amerika ya kusini na nchi za Karibbea ndizo ziliathiriwa mno. Idadi ya Wanyamapori katika kanda hizo ilipungua kwa 94% ndani ya miongo mitano iliyopita.

Ripoti hiyo imetoa mfano wa aina ya pomboo yaani dolphin wa rangi ya waridi wa Amazon nchini Brazil walipungua kwa asilimia 65 kati ya mwaka 1994 na 2016.

Ndovu na faru huenda wakapungua Tanzania

Andrew Terry ambaye ni mkurugenzi anayesimamia uhifadhi na sera katika chama hicho cha ZSL, amesema kupungua huko kwa idadi ya wanyama pori ni hali mbaya sana. "Inatuonesha kuwa asili ya ulimwengu inabaki tupu.”

Faru weupe ni miongoni mwa wanyama walioko katika hatari ya kuangamia kabisa ulimwenguni.
Faru weupe ni miongoni mwa wanyama walioko katika hatari ya kuangamia kabisa ulimwenguni.Picha: Parco Natura Viva/AFP

Terry ameongeza kuwa matokeo ya utafiti huo yanafanana na yale ya mwaka 2020 yaliyoonesha kuwa idadi ya wanyamapori inapungua kwa kasi ya 2.5% kila mwaka.

Imeshindikana kulinda wanyamapori?

Mark Wright ambaye ni mkurugenzi wa sayansi katika Mfuko wa Wanyamapori ulimwenguni  tawi la Uingereza amesema, asili ya ulimwengu ilikuwa katika hali mbaya na inazidi kuwa katika hali hiyo mbaya. "Bila shaka tunashindwa katika vita hivi,” amesema Wright.

Uhitaji Mkubwa wa Msaada

Licha ya hayo, ripoti hiyo pia ilionesha dalili za matumaini.WWF: Kuna kitisho kikubwa kwa viumbehai na bioanuwai duniani

Ingawa idadi ya sokwe katika mbuga ya kitaifa ya Kahuzi-Biega nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ilipungua kwa asilimia 80 kati ya mwaka 1994 na 2019, kwa sababu ya uwindaji kwa ulaji wa wanyamapori, idadi ya sokwe katika mbuga ya kitaifa ya Virunga iliongezeka kutoka takriban 400 mnamo mwaka 2010 hadi 600 mnamo mwaka 2018.

Juhudi za kuhifadhi na kuongeza idadi ya sokwe katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zazaa matunda.
Juhudi za kuhifadhi na kuongeza idadi ya sokwe katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zazaa matunda.Picha: DW

Ripoti hiyo imependekeza msaada zaidi kufadhili miradi ya kulinda na kuongeza idadi ya wanyamapori.

Nusu ya hifadhi za wanyama ziko hatarini

Wajumbe kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni watakutana- Montreal mwezi Disemba 2022, kujadili mkakati mpya wa ulimwengu wa kulinda mimea asili na wanyamapori.

Miongoni mwa maswali makubwa yanayotarajiwa kuulizwa ni jinsi ya kufadhili juhudi hizo za kiulimwengu.

Alice Ruhweza, mkurugenzi wa WWF kanda ya Afrika, amesema wanatoa miito kwa nchi tajiri kufadhili juhudi zao kifedha ili kulinda mazingira.

(RTRE)