ICC yaamuru waathiriwa wa Ongwen walipwe euro milioni 52
29 Februari 2024Wakitangaza hukumu yao, majaji wa ICC wamesema wanawake na watoto ndio waliopata madhara makubwa kabisa na ya kudumu kwa muda mrefu.
Jaji Bertram Schmitt amesema waathiriwa wa moja kwa moja wa mashambulizi, uhalifu wa kingono na kijinsia na watoto waliozaliwa kutokana na uhalifu huo pamoja na watoto waliotumikishwa jeshini walipata madhara makubwa na ya muda mrefu, yakiwemo ya kimwili na kiakili.
Majaji hao wameamuru fedha hizo zilipwe kwa pamoja na kuitaka Mfuko mahakama hiyo wa Waathirika kufanya mpango wa kuzilipa kwa sababu Ongwen, ambaye kwa sasa anatumikia kifuo chake katika gereza la nchini Norway, hawezi kulipa.
Soma pia: ICC kutoa uamuzi rufaa ya mbabe wa kivita wa kundi la LRA
Ongwen, ambaye mwenyewe alitekwa wakati akiwa na umri wa miaka tisa na kundi la waasi lililoongozwa na mtoro Joseph Kony, alipatikana na hatia mwaka wa 2021 na kuhukumiwa kifungo cha miaka 25 jela kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.
Uhalifu huo ulifanyika wakati Ongwen alikuwa sehemu ya kundi la Kony la LRA, ambalo liliendesha harakati zake kaskazini mwa Uganda katika miaka ya 2000.