1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yaikosoa Frontex kushiriki udhalilishaji wahamiaji Libya

13 Desemba 2022

Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch limeishutumu mamlaka inayosimamia mipaka ya Umoja wa Ulaya, Frontex, kwa udhalilishaji wanaofanyiwa wahamiaji wanaoteswa, kubakwa na hata kuuawa nchini Libya.

https://p.dw.com/p/4KqwG
Ocean Viking I Migranten aus dem Mittelmeer gerettet
Picha: Vincenzo Circosta/AA/picture alliance

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, wakala wa mipaka barani Ulaya, Frontex, umekuwa ukiitumia teknolojia ya ndege zisizo rubani kuwasaidia walinzi wa pwani ya Libya kuzikamata mashua za wahamiaji zinazovuuka Bahari ya Mediterenia kuelekea kusini mwa Ulaya, badala ya kuyasaidia mashirika ya kibinaadamu yanayoendesha operesheni za kuwaokowa wakimbizi wanaokabiliwa na hatari ya kuzama baharini. 

Mwaka jana pekee, watu zaidi ya 2,602 waliripotiwa kupoteza maisha ama kupotea wakiwa njiani kuelekea Ulaya kwa mashua, kwa mujibu wa mradi unaofuatilia wahamiaji wanaopotea unaofadhiliwa na Umoja wa Mataifa. 

Likitumia data zilizotolewa Alhamis iliyopita, shirika la Human Rights Watch lilisema siku ya Jumatatu (Disemba 13) kwamba mkakati wa Frontex "hauna umuhimu wowote katika kupunguza vifo vya wahamiaji, bali unaongeza idadi ya mashua zinazokamatwa na walinzi wa pwani wa Libya", ambapo maelfu ya wahamiaji wanaokamatwa na walinzi hao huteswa, kubakwa na hata kuuawa wakiwa mahabusu nchini Libya. 

"Kwa kuzipa taarifa mamlaka za Libya juu ya mashua zilizobeba wahamiaji, wakijuwa kuwa wahamiaji hao watakamatwa na kurejeshwa kwenye mateso, na licha ya kuwa na njia mbadala ya kufanya, Frontex ni sehemu ya udhalilishaji huu." Alisema mkurugenzi msaidizi wa Human Rights Watch, Juddith Sunderland.

Frontex yakanusha

Ocean Viking I Migranten aus dem Mittelmeer gerettet
Wafanyakazi wa shirika la uokozi la Ocean Viking wakiwasaidia wahamiaji waliokaribia kuzama kwenye Bahari ya Mediterenia.Picha: Vincenzo Circosta/AA/picture alliance

Wakala huo wa ulinzi wa mipaka ya Ulaya umekanusha tuhuma hizo ukiziita "taarifa zisizo sahihi." Lakini kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch, Frontex walianza kutumia ndege zisizo rubani kuchunguza pwani ya Libya kupitia kituo chake kilichoko nchini Malta mwezi Mei 2021. 

Baadaye, Frontex hutumia data inazopata kutoka ndege hizo kutambua mahala zilipo mashua zilizobeba wahamiaji wanaoelekea barani Ulaya na ndipo hapo hutumia taarifa hizo kuwajulisha walinzi wa pwani wa Libya wanaokwenda kuwakamata wahamiaji na kuwaweka kwenye vituo maalum.

Kwa kawaida vituo vilivyowekwa kuwashikilia kwa muda wahamiaji haramu vinapaswa kusimamiwa na serikali lakini makundi ya waasi yenye silaha ndiyo yanayozidhibiti. 

Umoja wa Ulaya umetowa zaidi ya dola milioni 500 kwa mamlaka nchini Libya kusaidia kuzuwia wimbi la wahamiaji wanaowania kuingia Ulaya. Fedha hizo zilizoanza kutolewa mwaka 2015 zinalenga kuimarisha ulinzi wa pwani kwa vifaa na mafunzo, na pia kuifanya hali ya vituo vya wahamiaji kuwa bora zaidi. 

Fedha za EU mikononi mwa wanamgambo

Mittelmeer Seenotrettung | Ocean Viking
Mashua ya wahamiaji ikiwa mkondoni kwenye Bahari ya Mediterenia kuelekea kusini mwa Ulaya.Picha: Jeremias Gonzalez/AP Photo/picture alliance

Lakini kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la AP mwaka 2019, sehemu kubwa ya fedha hizo imeangukia mikononi mwa wanamgambo na wasafirishaji haramu wa binaadamu.

Walinzi wa pwani pia wanafaidika na mpango huo, ambapo huwakabidhisha wahamiaji wanaowakamata baharini kwa wanamgambo kama sehemu ya biashara yao.

Shirika la Human Rights Watch liliyataka mataifa ya Umoja wa Ulaya kutuma meli zao wenyewe kwenye maeneo yale yale wanayotuma ndege zisizo rubani ili kuhakikisha kuwa wahamiaji wanaokamatwa hawaangukii mikononi mwa mamlaka za Libya.

Kwa miaka kadhaa sasa, mataifa ya Umoja wa Ulaya yamekuwa yakibishana juu ya nani mwenye wajibu wa kuwashughulikia wahamiaji wanaowasili kusini mwa Ulaya.

Hadi sasa, mataifa hayo yamekataa mpango wowote wa pamoja wa kuwatafuta na kuwaokowa wahamiaji yakisema utachochea wahamiaji zaidi kujaribu bahati yao ya kuingia barani Ulaya badala ya kupunguza.

Kila mwaka, maelfu ya wahamiaji wanaotarajia kufika Ulaya hupitia nchini Libya, taifa lililosambaratishwa kwa miaka kadhaa ya mapigano kati ya kambi hasimu za mashariki na magharibi, zinazoungwa mkono na makundi yenye silaha na hata serikali za mataifa ya kigeni.