UN yaeleza namna wakimbizi wanateseka kwenye mipaka ya Ulaya
28 Januari 2021Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR limezitaka nchi kuanzisha mfumo huru wa ufuatiliaji utakaohakikisha haki ya kutafuta hifadhi na kuchunguza ukiukaji.
Kamishna msaidizi wa masuala ya ulinzi wa UNHCR, Gillian Triggs amesema siku ya Jumatatu kuwa shirika hilo limepokea ripoti kadhaa kuhusu baadhi ya nchi za Ulaya zinazozuia upatikanaji wa hifadhi, zinazowarejesha wakimbizi baada ya kuingia ndani ya ardhi zao au kwenye maeneo yao ya bahari na kufanya ukatili dhidi yao kwenye mipaka.
Triggs amesema boti zinazowabeba wakimbizi zinarudishwa baharini na wahamiaji wengi wameripoti kufanyiwa vurugu na kunyanyaswa na vikosi vya baadhi ya nchi za Ulaya.
Wakimbizi wanakamatwa kiholela
Aidha, UNHCR limeonya pia kuwa wakimbizi wanaoingia kupitia mipaka ya nchi kavu wamelalamika kukamatwa kiholela na kulazimishwa kurejea kwenye nchi jirani, bila ya kuzingatia mahitaji yao ya kimataifa kuhusu ulinzi.
Hata hivyo, Triggs hakuitaja nchi yoyote kwa jina, ingawa siku za nyuma wakimbizi waliripoti vitendo vya aina hii vilivyofanywa na walinzi wa pwani wa Ugiriki.
Kwa mujibu wa UNHCR, wakimbizi na wahamiaji pia wamelishutumu shirika la ulinzi wa mipakani la Umoja wa Ulaya, Frontex kwa kushiriki katika kuwarudisha kinyume cha sheria.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema idadi ya wakimbizi wanaoingia Ulaya imepungua katika miaka ya hivi karibuni. Mwaka uliopita wa 2020 kulikuwa na wakimbizi 95,000 ambao ni sawa na asilimia 33, idadi hiyo ikiwa ni ya chini ikilinganishwa na ile ya mwaka 2018.
Soma zaidi: Idadi ya wakimbizi Ulaya yapanda juu kwa kasi
Wakati huo huo, shirika la Frontex linasitisha shughuli zake Hungary baada ya serikali kutotekeleza uamuzi uliotolewa mwezi Desemba na mahakama ya juu ya umoja huo, wa kutoa ulinzi wa kimataifa kwa watu wanaotafuta hifadhi.
Msemaji wa Frontex Chris Borowoski amesema uamuzi huo ambao haujawahi kufanyika, umechukuliwa kutokana na Hungary kushindwa kuheshimu uamuzi wa Mahakama ya Haki ya Ulaya, ECJ, ambao ulisema nchi hiyo haijatekeleza majukumu yake ya kutoa ulinzi wa kimataifa kwa waomba hifadhi.
Mahakama hiyo pia imebaini kuwa walinzi wa mipakani waliwarudisha kinyume cha sheria wahamiaji waliokuwepo Hungary bila ya kuwapa idhini ya kuingia nchi jirani ya Serbia, na hivyo kukiuka sheria za Umoja wa Ulaya zinazozitaka nchi wanachama kukubali na kutathmini maombi ya wakimbizi wanaotafuta hifadhi.
Shirika la UNHCR, limefafanua kuwa Mkataba wa Wakimbizi wa mwaka 1952, Mkataba wa Ulaya kuhusu Haki za Binaadamu na Sheria za Umoja wa Ulaya, zinayataka mataifa kulinda haki ya watu kutafuta hifdhi na ulinzi, hata ikiwa wameingia kwenye nchi husika kinyume cha sheria.
(AFP, AP)