Ulaya yalemewa na wakimbizi
19 Agosti 2015Idadi ya wahamiaji wanaoingia barani Ulaya imevunja rikodi kwa mwezi uliopita, ambapo wakimbizi laki moja, elfu saba na mia tano, wameripotiwa kuvuuka mipaka ya Umoja wa Ulaya. Mamlaka ya mipaka ya Ulaya, Frontex, inasema idadi hii inapindukia maradufu, ile ya wakimbizi 70,000 waliongia mwezi Juni. Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, miezi saba ya kwanza ya mwaka huu imeshuhudia takribani wahamiaji 340,000, wakiingia Ulaya kutoka ile ya wahamiaji 123,500, walioingia katika kipindi kama hiki, mwaka jana.
Mkurugenzi wa Frontex, Fabrice Leggeri, amesema sasa ni wazi Ulaya inatumbukia kwenye mzozo wa kibinaadamu na ametoa wito wa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya kuongeza msaada wao kwa mataifa yanayopokea mmiminiko huo wa wakimbizi kwenye mipaka yao. Takribani watu 2,000 wameshapoteza maisha mwaka huu pekee wakijaribu kuingia Ulaya, wengi wao kwenye Bahari ya Meditterenia, wa karibuni kabisa wakiwa wakimbizi 11 wa Syria waliokufa maji jana karibu Ugiriki wakitokea Uturuki.
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNCHR) linasema wiki iliyopita pekee wahamiaji 20,843 - wote wakiripotiwa kukimbia vita nchini Syria, Afghanistan na Iraq - waliwasili Ugiriki, ambayo kuanzia mwezi Januari hadi sasa imeshapokea wahamiaji 160,000.
Msemaji wa UNHCR, William Splinder, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa idadi imeongezeka zaidi katika kipindi cha wiki chache zilizopita, ambapo majira ya kiangazi yanakaribia ukingoni. Kote kwenye visiwa vya kusini na kaskazini ya Bara la Ulaya, wimbi la wakimbizi linaonekana kutokudhibitika.
Ujerumani yaelemewa
Ujerumani, taifa lenye nguvu kubwa kiuchumi barani Ulaya, inatazamia kupokea maombi 750,000 ya wakimbizi mwaka huu. Katika kila wakimbizi watatu wanaoingia Ulaya, mmoja huishia Ujerumani. Hapo jana, mkuu wa UNCHR, Antonio Gutteres, alitaka mshikamano zaidi baina ya nchi za Ulaya katika kuwachukuwa wakimbizi, akisema ni kinyume kwa Ujerumani na Sweden pekee kubeba wakimbizi wengi zaidi.
Kwa upande wao, Uingereza na Ufaransa zinajitayarisha kusaini mpango wa kupunguza makali mzozo wa wahamiaji katika mji wa kaskazini mwa Ufaransa, Calais, ambako maelfu ya watu wanaopigania kuingia Uingereza kupitia njia ya chini ya bahari wamekusanyika.
Hadi sasa hakuna dalili ikiwa idadi ya wakimbizi wanaoingia Ulaya inaweza kupungua. Katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha ZDF mwanzoni mwa wiki hii, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema huenda mzozo wa wahamiaji barani Ulaya ukawa ndio mkubwa zaidi kuliko wa madeni ya Ugiriki na uthabiti wa sarafu ya euro.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga