Frontex lakiuka haki za wakimbizi
6 Agosti 2019Zaidi ya hayo ripoti hiyo inasema shirika hilo la Frontex lenyewe limehusika mara kadhaa katika ukiukaji wa haki za binadamu.
Afisi ya habari ya shirika la Frontex huko Warsaw siku ya Jumatatu ilikuwa na shughuli nyingi. Msemaji wa shirika hilo Izabella Cooper aliahidi kwamba kutatolewa taarifa kamili. Baada ya muda taarifa hiyo ilitolewa na ilisema kuwa walinzi wa mipaka ambao wanaiunga mkono Frontex hawajahusika moja kwa moja katika matumizi ya nguvu au kuwarudisha wahamiaji makwao kinyume cha sheria.
Msemaji wa Halmashauri Kuu ya Ulaya anakiri kuwepo kwa stakabadhi za ukiukaji haki
Vyombo vya habari vya Bayerische Rundfunk na gazeti la The Guardian vimetoa ripoti yao iliyotokana na ripoti ya ndani ya shirika la Frontex inayoeleza kwamba maafisa wa mpakani kutoka Hungary, Bulgaria na Ugiriki waliwapiga wakimbizi na wahamiaji, wakawakimbiza kwenye misitu kwa kutumia mbwa na kuwasukuma kinyume cha sheria nje ya mipaka ambayo walikuwa washaivuka.
Msemaji wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Mina Andreeva amekiri kuwepo kwa stakabadhi zenye maelezo kama hayo.
"Kuna ripoti zilizowasilishwa katika bodi ya shirika. Hii inaonyesha kuwa kuna mkakati uliowekwa kuangalia iwapo na ni jinsi gani haki za binadamu zinaheshimiwa katika shughuli zote za Frontex. Nafikiri ni muhimu kutofautisha kati ya walinzi wa mipaka wa kitaifa na walinzi wa mipaka wa Ulaya kutoka shirika la Frontex," alisema Mina Andreeva.
Madai ya kwamba maafisa wa Frontex wanazikiuka haki za binadamu wakati wa kuwasafirisha na kuwarudisha katika nchi zao wahamiaji na wakimbizi, yamekanushwa kabisa na uongozi wake.
"Udhalilishaji wa aina yoyote wa wakimbizi na wahamiaji haukubaliki. Kwa sasa tutachunguza haya madai yote na walinzi wa mipaka wa Umoja wa Ulaya na tuchukue hatua zinazotakikana," aliongeza Mina Andreeva.
Keßler hashangazwi na ripoti za ukiukaji wa haki za Frontex
Mwenyekiti wa baraza la Frontex Stefan Keßlar ameiambia DW kuwa madai hayo hayakumshtua,kilichomshtua ni kwamba maafisa wa shirika hilo wamelaumiwa moja kwa moja.
Keßler amesema kwa mfano madai kwamba wakimbizi na wahamiaji katika mpaka wa Hungary hawaangaliwi vyema si jambo jipya kwani hata Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya iliipeleka Hungary katika Mahakama ya Haki ya Ulaya kwasababu hiyo hiyo.
Frontex lakini imeiambia DW kuwa hakujakuwa na malalamiko rasmia hata mara moja kuhusiana na shughuli zake za mpakani hata ingawa njia ya kuwasilisha malalamiko ni rahisi, kupitia tovuti yake tu.