1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sweden kuwaondoa wahamiaji waliokataliwa hifadhi

28 Januari 2016

Sweden inapanga kuwaondoa kiasi ya wahamiaji 80,000 ambao maombi yao ya kutaka wapewe hifadhi nchini humo yamekataliwa.

https://p.dw.com/p/1Hl7Y
Picha: Getty Images/AFP/J. Nilsson

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Sweden, Anders Ygeman amekaririwa na gazeti la kila siku la Dagens Industri akisema kiasi asilimia 45 ya maombi ya hifadhi yamekataliwa na nchi hiyo inatakiwa kujiandaa kuwarejesha maelfu ya wakimbizi 163,000 walioomba hifadhi nchini Sweden mwaka uliopita.

Amesema huenda watu 60,000 wakarudishwa lakini pia idadi hiyo inaweza ikafika 80,000 na kwamba wakimbizi hao watarejeshwa makwao kwa kutumia ndege ya kukodi na itatekelezwa kwa miaka kadhaa.

Polisi na maafisa wa uhamiaji wamepewa maelekezo ya kuandaa zoezi la kuwarejesha wakimbizi hao na kuna haja ya kuongeza askari zaidi pamoja na ushirikiano kati ya maafisa hao.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Sweden, Anders Ygeman
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Sweden, Anders YgemanPicha: picture-alliance/dpa/L. Dubrule

Wiki hii Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Lofven aliahidi kuongeza vitendeakazi kwa polisi ili kupambana na tatizo la kuzidiwa na majukumu kutokana na hali ya wakimbizi iliyopo.

Msemaji wa polisi wa jimbo la Magharibi mwa Sweden, Christer Fuxborg anasema, ''Kuna watu wengi wanakuja Sweden na hatujajiandaa kupokea watu wengi namna hii wanaowasili. Na hili ni tatizo kubwa kwa vikosi vya polisi na maafisa wa uhamiaji na jamii nzima kwa ujumla, na tunatafuta ufumbuzi mwingine wa kurejea katika utendaji wa kawaida tena.''

Ofisi zinazowaajiri watu wasio na kibali kushughulikiwa

Ygeman amesema maafisa pia wanatakiwa kujiandaa kuwashughulikia waajiri ambao wanawaajiri watu wanaoishi Sweden bila ya kuwa na kibali na kuhakikisha kwamba hawatoi hongo ili waendelee kuishi kinyume cha sheria.

Hayo yanajiri baada ya jana Umoja wa Ulaya kuikosoa Ugiriki jinsi inavyokabiliana na mzozo wa wakimbizi, ikisema nchini hiyo imekiuka jukumu lake la kuilinda mipaka ya Ulaya. Makamu Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Valdis Dombrovskis, amesema Ugiriki huenda ikakabiliwa na udhibiti wa mipaka kwa kushindwa kulinda mipaka ya mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya ambayo yako katika eneo la Schengen, iwapo hatua muhimu hazitachukuliwa.

Amesema rasimu ya ripoti imeonyesha Ugiriki imeshindwa kuwaandikisha wahamiaji ipasavyo na kuchukua alama zao za vidole, huku wasiwasi kuhusu usalama ukiendelea kuwa mkubwa baada ya kugundulika kwamba wapiganaji wawili wa jihadi wanahusika na mashambulizi ya kigaidi ya Paris, ambao waliingia Ulaya wakijifanya wakimbizi.

Boti iliyojaa wakimbizi Ugiriki
Boti iliyojaa wakimbizi UgirikiPicha: picture-alliance/dpa/S. Baltagiannis

Wakati huo huo, askari wa ulinzi wa pwani wa Ugiriki wamesema kiasi ya watu 11 wengi wao wakiwa watoto, wamekufa leo baada ya boti yao kuzama kwenye pwani ya kisiwa cha mashariki cha Ugiriki, Samos huku idadi ya watu isiojulikana wakiwa hawajulikani walipo.

Meli na boti za walinzi wa pwani kutoka Frontex, zinaendelea na zoezi la uokozi katika kisiwa hicho. Watu 10 walionusurika wameokolewa, huku miili ya wavulana wanne na wasichana watatu, wanaume watatu na mwanamke mmoja ikiwa imegundulika.

Boti nyingine ilizama jana kwenye kisiwa cha Kos na kusababisha vifo vya watu saba, wakiwemo watoto wawili. Watu wawili pekee ndiyo waliokolewa katika ajali hiyo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,DPAE,RTRE
Mhariri: Yusuf Saumu