Hong Kong yakumbwa na mafuriko makubwa
8 Septemba 2023Baadhi ya mitaa na vituo vya treni vimefurika maji hali ambayo imelazimisha shule kufungwa mjini humo. Katika mji jirani wa China Shenzhen, nje ya mpaka wa HongKong, mvua kubwa kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1952 imelirekodiwa.
Wataalam wanasema mabadiliko ya tabia nchi yameongeza vimbunga vya kitropiki huku mvua nyingi na upepo mkali unaosababisha mafuriko na uharibifu wa pwani vikishuhudiwa. Mvua kubwa imeripotiwa pia kunyesha usiku kucha kusini mwa China.
Mamlaka ya Hong Kong imesema wakati wa mkutano wa pamoja na wanahabari siku ya Ijumaa kwamba hali hiyo inatarajiwa kuendelea hadi angalau usiku wa leo. Mamia ya watu wamehamishwa na kupelekwa maeneo salama.
Video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha mitaa iliyofurika huko Hong Kong na katika mkoa wa karibu wa Guangdong, huku magari yakielea. Vikosi vya uokoaji vimekuwa vikitumia mitumbwi.
Mvua kubwa mjini Hong Kong ilianza Alhamisi hadi usiku wa manane. Kulingana na rekodi za wachunguzi wa hali ya hewa milimita 158.1 za mvua zilirekodiwa kila saa ikiwa ni rekodi ya juu zaidi tangu mwaka 1884 mjini humo.