Kifo cha Raisi: Waombolezaji watoa heshima za mwisho
21 Mei 2024Raia hao mamia kwa maelfu waliobeba bendera za taifa hilo na picha za Ebrahim Raisi wameshuhudiwa katika uwanja wa Central square mjini Tabriz wakitembea kando ya gari lililobeba majeneza ya Raisi na maafisa wengine saba.
Mji huo ndiko alikokuwa akielekea kiongozi huyo na ujumbe wake wakati helikopta waliyokuwa wakisafiria ilipopata ajali Jumapili. Mwili wa Raisi utasafirishwa kwa ndege kuelekea mji wa Qom na baadaye leo kabla ya kuelekea mji mkuu, Tehran, jioni.
Soma zaidi:Mokhber: Hakuna kitakachoharibika Iran
Maandamano makubwa ya kutoa heshima za mwisho na gwaride vitafanyika katika mji huo mkuu Jumatano asubuhi kabla ya Kiongozi Mkuu wa Kidini na Kisiasa wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei kuongoza ibada ya kumuaga.
Maziko ya Raisi kufanyika Alhamisi
Mwili wa Raisi unatarajiwa kusafirishwa baada ya hapo kuelekea nyumbani kwake katika mji wa Mashhad anakotarajiwa kuzikwa Alhamisi katika msikiti wa Imam Reza.
Raisi Ebrahim Raisi, waziri wake wa mambo ya kigeni Hossein Amir-Abdollahian na maafisa wengine, walipata ajali hiyo walipokuwa wakitokea katika uzinduzi wa mradi wa pamoja na Azerbaijan wa bwawa la kufua umeme katika mto Aras. Mto huo ni sehemu ya mpaka wa Azerbaijan na Iran na uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na Rais Ilham Aliyev.
Soma zaidi: Iran kufanya uchaguzi mkuu wa rais mnamo Juni 28
Helikopta iliyokuwa imembeba Raisi ilipoteza mawasiliano ilipokuwa ikirejea Tabriz baada ya shughuli hiyo. Televisheni ya taifa ya Iran ilitangaza kifo cha kiongozi huyo na abiria wote waliokuwa kwenye helikopta hiyo Jumatatu baada ya saa kadhaa za operesheni ya uokoaji. Tayari serikali ya Iran imeagiza uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali hiyo.
Soma zaidi: Rais wa Iran amefariki katika ajali ya helikopta
Kutokana na msiba huo, Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, alitangaza siku tano za maombolezo na ameshamthibitisha aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais Mohammad Mokhber, kuwa kaimu raisi. Kulingana na shirika la habari la Iran, uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaopaswa kufanyika ndani ya siku hamsini baada ya kifo cha Raisi, unatarajiwa kufanyikaJuni 28.