1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ibrahim Raisi:Rais aliekuwa mwandani wa Ayatollah Khamenei

20 Mei 2024

Ebrahim Raisi alikuwa rais wa Iran kwa takriban miaka mitatu. Ingawa Kiongozi Mkuu Ali Khamenei ndiye mwenye usemi wa mwisho katika masuala yote ya kimkakati, uwezo na ushawishi wake ulikuwa mkubwa.

https://p.dw.com/p/4g4IS
Iran Teheran | Aliekuwa Rais wa Iran Ebrahim Raisi
Rais Ebrahim Raisi amefariki dunia baada ya kuiongoza Iran kwa takribani miaka mitatu.Picha: Iranian Presidency/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Ebrahim Raisi, aliyefariki Jumapili katika ajali ya helikopta, alifanya kazi katika mahakama ya Iran kwa zaidi ya miongo mitatu kabla ya kuapishwa kuwa rais mnamo Agosti 2021.

Raisi mwenye umri wa miaka 63 alikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na, wachambuzi wanasema, alikuwa na uhusiano wa karibu na Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, mtu mwenye nguvu zaidi nchini humo.

Raisi aliyezaliwa mwaka wa 1960 huko Mashhad, kaskazini-mashariki mwa Iran, alishinda uchaguzi wa rais mwezi Juni 2021 kwa kupata chini ya asilimia 62 ya kura kama mgombea mkuu wa wanasia wa mrengo mkali wa kisiasa na mgombea aliependelewa na mwanafunzi wa Khamenei.

Soma pia: Iran yaomboleza kifo cha Rais wake

Uchaguzi huo uliitikiwa na idadi ndogo ya wapiga kura ya takriban asilimia 48.9 tu katika nchi yenye watu milioni 83, rekodi ya chini kabisaa katika historia ya miaka 42 ya Jamhuri ya Kiislamu. Raisi alimrithi Hassan Rouhani mwenye msimamo wa wastani, ambaye alizuwiwa kuwania muhula mwingine kutokana na sheria ya ukomo wa mihula, baada ya kuongoza kwa mihula miwili.

Ajali ya Helikopta ya Iran. Rais Ebrahim Raisi aliuawa kwenye ajali hiyo
Mahujaji wa Kishia wakiomba baada ya kifo cha RAis Ebhrahim Raisi katika ajali ya Helikopta.Picha: Alaa Al-Marjani/REUTERS

Katika miongo mitatu aliyofanya kazi katika mahakama ya Irani, Raisi alihudumu kwanza kama mwendesha mashtaka kwanza, baadaye kama jaji na, tangu 2019, kama mkuu wa mahakama. Raisi alitajwa kuhusika na kufungwa, na hata kuwanyonga wapinzani kadhaa wa Iran alipokuwa mwendesha mashtaka mkuu. Alikanusha shutuma hizo mara kadhaa wakati wa kampeni za urais.

Nguvu yake ndani ya mfumo tawala

Kwa mujibu wa katiba ya Iran, licha ya cheo cha rais, Raisi alikuwa nambari mbili katika muundo wa mamlaka ya nchi kwa sababu Khamenei anafanya kazi kama mkuu wa nchi na ndiye mwenye uamuzi wa mwisho katika masuala yote ya kimkakati. Pia ni kamanda mkuu wa majeshi ya Iran.

Katika msimu wa mapukutiko wa mwaka 2022, kifo cha mwanamke wa Kikurdi wa Irani Mahsa Amini kilisababisha maandamano makubwa nchini Iran. Mwanamke huyo kijana aliefariki akiwa mikononi mwa polisi baada ya kukamatwa na polisi wa maadili kwa kukiuka kanuni za mavazi ya Kiislamu.

Soma pia:Risala za rambirambi zatolewa kutoka kote duniani kutokana na kifo cha Rais wa Iran Ebrahim Raisi 

Makumi kwa maelfu waliandamana kote nchini dhidi ya sera za ukandamizaji za serikali na mfumo wa utawala wa Kiislamu. Vikosi vya usalama na utekelezaji wa sheria chini ya Raisi vilijibu kwa vurugu na mashtaka makali. Makumi ya maelfu ya waandamanaji walikamatwa.

Iran| Ebrahim Raisi enzi za ujana wake
Ebrahim Raisi enzi za ujana wakePicha: donya-e-eqtesad.com/

Maandamano hayo yaliutumbukiza uongozi wa kisiasa katika mgogoro wake mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa.

Marekani na Umoja wa Ulaya mara kadhaa zimeiwekea vikwazo Iran - kwa ukiukaji wa haki za binadamu, lakini pia kwa sababu ya uungaji mkono wa Iran wa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.

Wakati huo huo, kuna wasiwasi mpya juu ya mpango wa nyuklia wa Iran. Mazungumzo ya kimataifa ya nyuklia na Tehran yamekwama na chini ya serikali ya Raisi uhusiano na nchi za Magharibi umezorota zaidi.

Iran pia ina uhasama mkubwa na Israel. Mnamo mwezi Aprili, Tehran iliishambulia Israeli kwa mara ya kwanza sio kupitia washirika wa kikanda kama vile waasi wa Kihouthi nchini Yemen au wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon, bali moja kwa moja - kujibu shambulio la bomu dhidi ya ubalozi wa Iran katika mji mkuu wa Syria Damascus.

Chanzo: dpae