1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres ziarani Kenya kujadili hali Sudan

Thelma Mwadzaya3 Mei 2023

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres ameanza ziara ya siku mbili nchini Kenya. Ajenda inajikita katika hali ya kibinadamu na usalama nchini Sudan ambako mapigano yanaendelea kati ya majeshi hasimu

https://p.dw.com/p/4Qr0r
UN Generalsekretär Antonio Guterres
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Senosi

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres aliwasili mapema Jumatano na kupokelewa na waziri wa mambo ya kigeni Alfred Mutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA. Ajenda ya ziara ya Guterres inajikita katika mzozo wa Sudan iliyotumbukia kwenye vita tangu katikati ya Aprili mwaka huu. Akizungumza jijini Nairobi, Guterres aliusisitizia umuhimu wa risasi kukoma kurindima Sudan.

Soma pia: Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kiutu awasili Port Sudan

Wakati wa mchana, Katibu Mkuu huyo alikutana na wafanyakazi wake katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa iliyoko jijini Nairobi, UNON alikofanya kikao na waandishi wa habari. Kadhalika anapanga kuhudhuria mkutano wa kwanza wa uratibu wa maafisa wakuu watendaji wa Umoja wa Mataifa hapo Alhamisi na Ijumaa.

Ägypthen Sudan l Ankunft Geflüchteter in Kairo
Malefu ya watu Sudan wamekimbilia nchi jiraniPicha: Amr Abdallah Dalsh/REUTERS

Ziara ya Antonio Guterres itampeleka pia hadi eneo la maziwa makuu atakakohudhuria mjini Bujumbura, kongamano la 11 la viongozi wa ngazi ya juu wa uangalizi wa mifumo ya amani,usalama na ushirikiano mintarafu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na eneo zima.

Soma pia: Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu mgogoro wa wakimbizi Sudan

Jioni hii ameandaliwa karamu maalum kwenye ikulu ya Nairobi na Rais William Ruto. Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR linakadiria kuwa kiasi ya watu laki moja wamekimbia mapigano Sudan na kukimbilia nchi jirani. Rais William Ruto alikuwa na haya ya kusema kuhusu hali ya Sudan mapema hii leo.

Ziara hii inafanyika wakati ambapo tofauti za kidiplomasia ziliibuka baada ya hati za siri za Marekani kuvuja. Duru zinaeleza kuwa mwezi wa Februari, mazungumzo ya binafsi kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na naibu wake Amina Mohamed yaliashiria kuwa yanadukuliwa na kwamba hana imani na kiongozi wa Kenya.

Hata hivyo hakuna thibitisho lililotolewa kuhusu muktadha wa kauli hizo au iwapo yalikuwa mazungumzo ya binafsi au rasmi. Kwa upande wake Umoja wa Mataifa uliweka bayana kuwa hauna tashwishi na uongozi wa Kenya.

Itakumbukwa kuwa Nairobi ni makao makuu ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, UNEP, pamoja na ofisi za kusimamia operesheni muhimu za mashirika yake makubwa.