1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres ahimiza kusitishwa mapigano kuruhusu misaada Gaza

21 Oktoba 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa mwito wa kusitishwa mapigano ili kuruhusu shughuli za utoaji msaada wa kiutu kwenye Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4Xr6Z
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihudhuria mkutano wa amani wa Cairo Picha: Khaled Desouki/AFP/Getty Images

Guterres ametoa matamshi hayo mbele ya mkutano wa kimataifa uliotishwa na Misri kujadili njia za kumaliza vita kati ya Israel na kundi la Hamas na kufungua mlango wa majadiliano ya amani.

Mkutano huo ulifunguliwa mapema siku ya Jumamosi saa chache baada ya msafara wa kwanza wa malori ya msaada wa kiutu kuvuka mpaka wa Rafah na kuingia Ukanda wa Gaza.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa ameorodhesha malengo matatu yanayopaswa kupewa kipaumbele hivi sasa.

Ameyataja kuwa ni kuondoa vizuizi katika usambazaji msaada wa kiutu, kuachiwa huru kwa watu wote waliochukuliwa mateka ndani ya Israel na kupunguza machafuko kuepusha mzozo huo kuwa wa kanda nzima.

Mkutano wa mjini Cairo uliopewa jina la "Kongamano la Cairo kwa ajili ya amani" umefanyika chini ya kiwingu cha wasiwasi kuwa mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa kundi la Hamas wanaotawala Gaza yanaweza kusambaa na kuwa mzozo wa kanda yote ya Mashariki ya Kati.

Guterres azungumzia suluhu ya mataifa mawili akisema muda "ni sasa"

Viongozi waliohudhuria mkutano wa amani ya Mashariki ya Kati mjini Cairo
Viongozi waliohudhuria mkutano wa amani ya Mashariki ya Kati mjini Cairo Picha: The Egyptian Presidency/REUTERS

Guterres amesema kwa maoni yake mzozo uliopo utatatuliwa chini ya msingi wa kuundwa madola mawili kwa maana ya Israel na taifa la Palestina.

"Wakati wa kuchukua hatua umewadia, kufanya kazi ya kumaliza kizaazaa hichi cha kutisha" amesema Guterres mbele ya viongozi wa mataifa mengi ya kiarabu, wawakilishi wa madola ya magharini pamoja na China waliokusanyika mjini Cairo.

Hata hivyo mkutano huo haujahudhuriwa na Marekani -- mshirika muhimu wa Israel -- wala Iran -- muungaji mkono mkubwa wa kundi la Hamas-- linalotawala Gaza.

Katika hotuba yake ya ufunguzi mwenyeji wa mkutano huo rais  Abdel Fattah El-Sisi wa Misriamesema ameitisha mkutano huo kutafuta makubaliano ya njia za kumaliza hali mbaya ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza na kufufua mchakato wa kusaka amani kwa mzozo kati ya Israel na Wapalestina.

Msaada wa kwanza wa kiutu waingia Ukanda wa Gaza

Wakati huo huo malori 20 yaliyobeba msaada wa kiutu yameingia Ukanda wa Gaza leo Jumamosi kupitia mpaka wa Rafah uliopo upande wa Misri.

Mkuu wa Misaada ya Kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amesema ana matumaini "kuwa shehena hiyo itakuwa ni mwanzo wa juhudi endelevu za kupeleka mahitaji muhimu ... kwa watu wa Gaza" na kutahadharisha lakini kwamba "msafara huo wa kwanza haupaswi kuwa wa mwisho."

Shehena ya kwanza ya msaada wa kiutu ikivuka mpaka wa Rafah kuingia Gaza
Shehena ya kwanza ya msaada wa kiutu ikivuka mpaka wa Rafah kuingia Gaza Picha: Mahmoud Khaled/Getty Images

Shehena hiyo ni ya kwanza tangu kuzuka kwa vita wiki mbili zilizopita kati ya Israel na kundi la Hamas, wanagambo wa kiislamu wanaotawala Ukanda wa Gaza wenye watu wapatao milioni 2.4.

Kivuko cha Rafah ndiyo ujia pekee wa kuingia Gaza ambao hauko chini ya udhibiti wa Israel, ambayo iliridhia kutumwa kwa msaada wa kiutu kutokea Misri baada ya ombi kutoka kwa Marekani, iliyo mshirika mkuu wa dola hiyo.

 Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema "hiyo ni hatua muhimu ya kupunguza madhila kwa watu wasio na hatia"

Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani amesifu taarifa za kuwasili kwa msaada wa kiutu Ukanda wa Gaza akisema ni "habari njema" na kwamba Ujerumani itafanya kazi "kupitia njia zote kuondoa mateso yaliyosababishwa na mzozo huu".

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uingereza James Cleverly amesema kuwasili kwa msaada Gaza hakupaswi kuwa jambo la mara moja na badala yake malori zaidi lazima yaruhusiwe siku zinazokuja.