Guterres ataka usitishwaji mapigano Gaza kwa sababu za kiutu
20 Oktoba 2023Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Ukanda wa Gaza unahitaji msaada wa kutosha na wa kudumu. Akizungumza mjini Cairo pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Sameh Shoukry, Guterres pia ametoa wito wa usitishaji mapigano mara moja kwa ajili ya misaada ya kiutu. Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa yuko Cairokutazama maandalizi ya msaada utakaopelekwa kwa Wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza.
Rais wa Marekani Joe Biden amesema malori machache yataruhusiwa kuingia katika Ukanda huo kutokea Misri kuanzia leo Ijumaa. Kwenye uwanja wa vita, Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amewataka wanajeshi wa nchi hiyo walioko kwenye mpaka wa Gaza kuwa tayari kuingia katika Ukanda huo, akidai kuwa wataanza kuiona Gaza kutokea ndani, na kuongeza kuwa amri inakuja. Wakati huo huo, familia za raia wa Ujerumani ambazo jamaa zao wamechukuliwa mateka na kundi la Hamas, wameitaka serikali mjini Berlin kufanya juhudi za ziada kuhakikisha mateka hao wanarejea salama, wakionya kuwa muda unayoyoma.