Guterres atembelea mpaka wa Rafah kuhimiza msaada kwa Gaza
20 Oktoba 2023Guterres aliwasili kwenye eneo la mpaka wa Rafah mapema leo mchana baada ya kufanya mazungumzo na maafisa wa serikali ya Misri mjini Cairo.
Alifika eneo hilo kujionea hali ilivyo na kushinikiza kufunguliwa kwa eneo hilo la mpaka kuruhusu malori la misaada ya kiutu kuvuka kuingia Gaza.
Alitoa hotuba akiwa amezingirwa na waandamanaji wa Misri waliokuwa wakipaza sauti za kuwaunga mkono Wapalestina.
Kiongozi huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ni muhimu kwa mpaka wa Rafah kufunguliwa akisema malori yaliyokwama kwenye eneo hilo yanabeba matumaini ya uhai kwa maisha ya mamilioni ya watu waishio Gaza.
"Tunahitaji. Kwa hakika tunahitaji malori haya yaruhusiwe haraka na kwa wingi iwezekenavyo. Lakini kufanikisha hilo tunahitaji juhudi endelevu. Hatutazamii kuwe na msafara mmoja pekee. Tunataka misafara mingi ipewe ruhusa ya kuingia Gaza kutoa msaada wa kutoza kwa watu Gaza" amesema Guterres.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaonya muda unayoyoma kufikisha msaada Ukanda wa Gaza
Eneo hilo la mpaka wa Rafah linatizamwa kwa karibu tangu Israel ilipoanza operesheni yake ya kijeshi ya kuishambulia Gaza kujibu shambulizi kubwa lililofanywa na kundi la Hamas linalotawala ukanda huo ndani ya ardhi ya Israel.
Tangu tukio hilo la Oktoba 7 Israel imeweka zuio kali la kuingizwa mahitaji muhimu kwenye Ukanda wa Gaza ikiwemo chakula, dawa na mafuta.
Mpaka wa Rafah eneo pekee lenye njia ya kuingia Gaza ambalo haliko chini ya udhibiti wa Israel ndiyo unatizamwa kuwa muhimu katika kufanikisha dhamira ya kupelekwa mahitaji ya kiutu ndani ya Gaza.
Kulikuwa na matumaini kuwa shehena ya kwanza ya misaada ingeruhusiwa kuanza kuingia leo baada ya kupatikana makubaliano yaliyofanikishwa na rais Joe Biden wa Marekani.
Hata hivyo hakuna lori lililovuka mpaka kwa sababu mamlaka za Misri zimesema zinahitaji kufanya ukarabati mkubwa wa barabara zilizoharibiwa na makombora ya Israel.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yametahadharisha kuwa muda unayoyoma kuwasaidia wakaazi wa Gaza wanaotaabika kwa kukosa mafuta, chakula, maji na hata madawa.
Maafisa kadhaa wa Misri na Umoja wa Mataifa wamesema kuna matumaini mpaka wa Rafah utafunguliwa kesho lakini hakuna uhakika iwapo mamia ya malori ya misaada yaliyokwama eneo hilo yataruhusiwa yote kuvuka na kuingia Gaza. Israel imesema inataka msaada unaopelekwa Gaza uwafikie raia pekee na siyo kundi la Hamas.
Jeshi la Israel laendelea kuishambulia Gaza huku ikiwa kwenye tahadhari mpaka wake na Lebanon
Jeshi la Nchi hiyo limendelea hii leo kuyashambulia maeneo chungunzima ya ukanda huo kuhujumu kile imekitaja kuwa maeneo ya maficho ya kundi la Hamas inalolenga kulitokomeza.
Jeshi hilo limesema tangu alfajiri imeyalenga karibu maeneo 100 yanayohusishwa na Hamas, kundi linalotawala Ukanda wa Gaza ambalo Israel na mataifa kadhaa ya magharibi yameliorodhesha kuwa la kigaidi.
Kwa upande mwingine kuna kitisho cha mzozo huo kuvuka mpaka na kuhusisha nchi jirani. Israel imekuwa kwenye hali ya tahadhari kubwa kwenye mpaka wake na Lebanon ambako wanamgambo wa Hezbollah wamekuwa wakifyetua makombora kuelekea Israel.
Viongozi wa mataifa ya magharibi wamekuwa njiani kutoka nchi moja kwenye nchi katika kanda ya Mashariki ya Kati kujaribu kwa kila hali kuzuia mzozo kati ya Israel na Palestina usigeuka kuwa wa kanda nzima.
Baerbock aitembelea Lebanon wakati Misri inaandaa mkutano kujadili mzozo wa Gaza
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock alikuwa mjini Beirut leo kuzungumza na maafisa wa Lebanon kwa dhima ya kuepusha kutanuka kwa mvutano kati ya nchi hiyo na Israel.
Alikutana na waziri wa mambo ya nchi za nje Abdallah Boi Habib na alipangiwa kuwa na mazungumzo na waziri mkuu wa mpito pamoja na mkuu wa majeshi akinuwia kuwanasihi wazungumze na Hezbollah kuepusha kundi hilo kujiunga kwenye mzozo wa Gaza na Israel.
Hapo kesho ataelekea Misri kushiriki mkutano wa kimataifa uliotishwa mjini Cairo kujadili mzozo unaoendelea na kutafuta suluhu ya kusitisha mapagano.
Maafisa kadhaa wa mataifa ya magharibi, yale ya kiarabu na viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wamethibitisha kuhudhuria mkutano huo.
Hata hivyo Marekani haitotuma wawakilishi wake hali iliyoibua mashaka juu ya kile kitakachofanikiwa kwenye mkutano huo.