1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Antonio Guterres atahadharisha elimu yaigawa dunia

Josephat Charo
20 Septemba 2022

Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafia Antonio Guterres ametahadharisha kuwa elimu inageuka kuwa nyenzo inayoigawa dunia kwa kasi, wakati akijaribu kuyaweka maendeleo katika ajenda ya mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa

https://p.dw.com/p/4H5I1
UN-Generalsekretär Guterres
Picha: Xie E/XinHua/dpa/picture alliance

Katika kikao maalumu wa kilele kuhusu elimu kabla viongozi wa dunia kukutana kwa mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kila mtu anafahamu elimu huyabadili maisha, uchumi na jamii mbalimbali lakini tunafahamu pia kwamba lazima tuifanyie mageuzi kwa sababu elimu iko katika mgogoro mkubwa. Amedokeza kuwa kiasi asilimia 70 ya wanafunzi wenye umri wa miaka kumi katika nchi masikini hawawezi kusoma. Ima hawaendi shule au wako shule lakini hawasomi vizuri.

"Elimu inageuka kwa kasi kuwa nyenzo kubwa inayosababisha mgawanyiko.  Mifumo ya elimu haizingatii sana kwamba elimu haina mwisho na walimu hawajapokea mafunzo wakahitimu vizuri, hawathaminiwi na wanalipwa mishahara midogo. Na pengo la ufadhili wa elimu linaendelea kutanuka kuliko ilivyowahi kushuhudiwa."

Guterres ameutahadhirisha mkutano kwamba janga la ugonjwa wa Covid-19 lilisababisha athari kubwa kwa elimu, huku wanafunzi maskini wakikosa teknolojia na mizozo ikitatiza masomo shuleni. Amezitolea wito nchi zote zitoe kipaumbele kuongeza matumizi ya fedha kwa kila mwanafunzi huku kukiwa na maswali mengi kuhusu uchumi wa dunia.

Elimu ya wasichana iimarishwe

Katika ripoti iliyochapishwa mapema mwezi huu shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP lilisema ugonjwa wa Covid-19 ulirudisha nyuma maendeleo ya binadamu kwa miaka mitano. Guterres pia aliutaka utawala wa Taliban nchini Afghanistan ufute vikwazo vyote kuhusu elimu kwa wasichana na iwaruhusu waendelee na masomo katika shule za sekondari.

Malala Yousafzai | Sao Paulo, Brazil
Malala YousafzaiPicha: Miguel Schincariol/AFP/Getty Images

Akizungumza katika mkutano huo mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2014 ambaye pia ni balozi wa amani wa Umoja wa Mataifa, Malala Yousafzai, amezitaka nchi zenye kipato cha juu ziongeze misaada, zifuteni madeni na ziweke mifumo ya haki ya kimataifa ya kodi ili nchi zenye kipato cha chini ziweze kutumia fedha zaidi kwa ajili ya wasichana.

"Msitoe ahadi ndogo za choyo na za muda mfupi. Jitoleeni kuilinda haki ya kupata elimu kamili na kuondosha kabisa pengo la ufadhili. Tumieni mamlaka mliyonayo kuchukua hatua. Tengeni asilimia 20 ya bajeti zenu kwa elimu.

Mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa unafanyika baada ya miaka miwili ya janga la corona, huku viongozi wakitakiwa kuhudhuria vikao mjini New York ikiwa wanataka kuhutubia, isipokuwa rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky. Hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa ilipiga kura kumruhusu rais Zelensky, ambaye anaongoza upinzani dhidi ya uvamizi wa Urusi, ahutubie bila kufika New York.

(afpe)