Guterres aitaka Taliban kuruhusu wasichana kusoma
19 Septemba 2022Guterres amesema Jumatatu hii kwamba " kutoka kwenya jukwaa hili ninaziomba mamlaka nchini Afghanistan kuondoa mara moja vizuizi vyote vinavyozuia wasichana kupata elimu ya sekondari." Guterres amesema hayo leo, wakati mkutano wa kilele wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.
Tangu kurejea kwenye mamlaka mwaka 2021, Taliban imewazuia wasichana kusoma zaidi ya darasa la sita, hatua iliyoibua mjadala wa kitaifa na iliyowasikitisha wasichana wengi.
Soma Zaidi: Wanawake wameathirika zaidi katika utawala wa Taliban
Zuio hilo linaongeza kitisho cha kutengwa zaidi, machafuko na mateso dhidi ya wasichana, imesema sehemu ya taarifa iliyochapishwa na Umoja wa Mataifa. Taarifa hiyo imesema kuwawezesha wasichana kurejea shuleni kutatoa matumaini mapya kwa watu wake, ingawa kwa upande mwingine umoja huo unaonyesha wasiwasi kwamba kuendelezwa kwa hatua kama hizo kutaongeza mzozo uliopo nchini humo.
Taliban wenyewe wamesema kwamba wasichana wanaosoma shule za sekondari wanaweza kuruhusiwa kurejea madarasani kuanzia darasa na saba na kuendelea lakini kukiwa na masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na wasichana hao kuvaa vazi la kiislamu "hijab" pamoja na kufundishwa na walimu wa kike katika majengo tofauti.
Utawala wa Taliban umekabiliwa na majanga kadhaa ikiwa ni pamoja na mashambulizi makubwa yanayofanywa na wanamgambo wanaojiita Dola la Kiislamu, IS, sambamba na umasikini, ukosefu wa ajira, uhamiaji na hata majanga ya kiasili ambavyo kwa pamoja viezidi kuliathiri taifa hilo lililoathiriwa kwa vita.
Hadi sasa hakuna taifa lililoitambua serikali hiyo ya Taliban.
Mashirika: DPA