Rwanda yaanza ujenzi wa kiwanda cha chanjo ya Covid 19
23 Juni 2022Scholz aliyasema hayo alipokuwa akihutubia kwa njia ya mtandao hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza chanjo mbalimbali ikiwemo ile ya corona mjini Kigali nchini Rwanda. Hafla hiyo ni kabla ya kuanza mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Madola.
Kuweka jiwe la msingi katika eneo lililotengwa maalum kwa ajili yaujenzi wa viwanda vya kutengeneza chanjo na kituo cha kimataifa kwa ajili ya utafiti katika chanjo nyingine za aina mbalimbali ni mwanzo wa utekelezwaji wa mkakati wa umoja wa Afrika wa kuhakikisha asilimia 40% ya chanjo zinazohitajika barani Afrika ziwe zitanatengenezwa barani humo ifikapo mwaka 2040.
Mgao sawa wa chanjo ni tatizo kubwa ulimwenguni
Kansela Scholz alisema kuweka jiwe hilo la msingi la kiwanda hicho ni suluhu katika tatizo lililopo sasa la mataifa kushindwa kupata mgao sawa kwenye suala la chanjo.
"Janga la corona limeonyesha kwamba mgao sawa kwa chanjo za Corona mpaka sasa ni tatizo ulimwenguni. Kwa hali hiyo mikakati kuelekea kutatua hilo ndiyo njia sahihi, hii inakwenda na kampeni inayofanywa na Ujerumani kwa sasa ya kupata chanjo kwa mataifa yote ulimwenguni Tumesema hapo mwanzo na sasa tunasema tena kwamba janga lolote linaweza kuisha endapo watu wote watawezeshwa kupata chanjo," alisema Scholz.
Rais wa Ghana Akufo Nana Addo alisema wakati umefika Afrika iwe mstari wa mbele kutafuta suluhu la matatizo hasa haya ya majanga na magonjwa mbalimbali, lakini hilo litawezekana endapo mataifa yatashirikiana.
"Umuhimu wa mradi mkubwa kama huu ni kwamba tunapaswa kufanya kazi pamoja, na ndiyo maana kesho tarehe 24 mwezi huu taasisi za uratibu wa vyakula na madawa za Rwanda na Ghana zitatia saini mkataba wa ushirikiano. Kupitia mkataba huu taasisi ya uratibu wa madawa na vyakula ya Ghana ambayo inatambuliwa na shirika la afya ulimwenguni kama iliyoko katika kiwango cha tatu katika ubora…itasaidia taasisi ya uratibu wa madawa na vyakula ya Rwanda kufikia hatua hii haraka iwezekanavyo," alisema Rais Addo.
Ujenzi wa kiwanda cha chanjo ni hatua kubwa kuelekea usawa wa chanjo
Ujenzi wa viwanda vya kuzalisha chanjo ya Corona utafanyika katika nchi za Rwanda, Senegal, Ghana na Afrika Kusini kwa mujibu wa azimio la umoja wa Afrika.
Rais Paul Kagame wa Rwanda alisema Rwanda itahakikisha inaweka mazingira bora na mahitaji mengine ya kuinua kiwango cha uwekezaji katika taasisi kubwa katika sekta nyingine
"Kuweka jiwe hili la msingi ni hatua kubwa kuelekea hatua nzuri ya mgao sawa wa chanjo kwa wote. Rwanda inanuia kutumia mradi huu kwa kuhakikisha mazingira bora na rahisi kuwamasisha wawekezaji wengine wakubwa kuja kuwekeza kwenye sekta nyingine. Hapa tuliposimama ni eneo ambalo tumeamua liwe la uwekezaji katika sekta ya madawa na Rwanda inaendelea kushirikiana na wadau wengine shirika la fesha la kimataifa na benki ya uwekezaji ya ulaya kuhakikisha haya yanafanikiwa," alisema Kagame.
Kuanzia Ijumaa hadi Jumamosi wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola watakuwa katika mkutano wa faragha katika ukumbi wa Kigali convention Center mjini Kigali.
Tayari viongozi mbalimbali wamekwishafika na mapema Alhamis alifika waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson pamoja na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.