1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIndia

G20: Nchi maskini duniani kupata afueni ya madeni?

17 Julai 2023

Mawaziri wa fedha na wakuu wa benki kuu katika nchi 20 zilizostawi kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi G20, Jumatatu huko nchini India, wanaanza mazungumzo ya kurekebisha mikataba ya ulipaji madeni.

https://p.dw.com/p/4Tyko
Indien Gandhinagar | vor G20-Treffen der Finanzminister | Weltbank-Chef Ajay Banga
Mkuu wa Benki ya Dunia Ajay Banga akiwa Gandhinagar, India kwa ajili ya G20Picha: SAM PANTHAKY/AFP

Mazungumzo hayo pia yatakuwa yanajikita katika makubaliano yenye usawa, ya kodi za kimataifakwa lengo la kuuinua uchumi wa dunia unaonywea.

Mkutano huo wa siku mbili katika mji wa Gandhinagar, unaongozwa na waziri wa fedha wa India Nirmala Sitharaman, anayesema, eneo linalotarajiwa kuwa na majadiliano mapana ni hali ya uchumi wa dunia.

Cha muhimu kitakachokuwa katika ajenda hiyo ya siku mbili ni juhudi za kukabiliana na dhiki ya ulipaji madeni, huku nchi maskini zaidi duniani zikiathirika zaidi na mzozo wa madeni duniani, katika wakati ambapo nchi hizo zinahitaji fedha zaidi kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

China hairidhii makubaliano yoyote ya urekebishaji madeni

Maafisa lakini wanasema China, ambayo ndiyo nchi yenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani na mkopeshaji mkubwa wa fedha kwa nchi kadhaa maskini barani Afrika na Asia, imekataa makubaliano yoyote ya pamoja yatakayoafikiwa kuhusiana na suala hilo la kurekebisha madeni. China imekosolewa mno kwa msimamo wake huu.

Indien Gandhinagar | vor G20-Treffen der Finanzminister | US-Finanzministerin Yellen
Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen akiwa Gandhinagar, IndiaPicha: SAM PANTHAKY/AFP

Akizungumza pembezoni mwa mkutano huo wa G20, waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen, ametoa mfano wa urekebishaji wa deni la Zambia, jambo alilolizungumzia alipokuwa ziarani beijing mwezi huu. Yellen amesema majadiliano kuhusiana na deni la Zambia yamechukua muda mrefu na akaongeza kuwa, anatarajia mazungumzo kuhusu madeni ya Ghana na Sri Lanka yatakamilika hivi karibuni.

Waziri huyo wa fedha wa Marekani ametaka msingi uliotumika katika kurekebisha deni la Zambia utumike katika madeni mengine yote, badala ya kuanza mwanzo kwa kila nchi inayojadiliwa.

Yellen ameongeza kwamba zaidi ya nusu ya nchi zote zenye kipato cha chini zinakaribia au tayari zishaingia katika matatizo ya ulipaji madeni, hiyo ikiwa ni mara mbili ya hali ilivyokuwa mwaka 2015. Kauli hii ya Yellen imeungwa mkono na afisa mmoja mwandamizi kutoka kwa mwenyeji wa mkutano huo India.

Hatua ya kwanza ya mapato ya makampuni kutangazwa

Nchi hizo za G20 pia zitajadili mabadiliko ya taasisi za kimataifa za fedha, sarafu za kidijitali na mikakati ya kurahisisha upatikanaji wa fedha kwa nchi maskini, kwa ajili ya kukabiliana na madhara yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mkutano wa kilele wa G20 waanza Japan

Hatua mpya ya kwanza kuhusiana na usambazaji wa mapato yanayotokana na kodi kutoka kwa makampuni yaliyo na matawi katika nchi nyingi, iliyofikiwa na nchi 138 wiki iliyopita, inatarajiwa kutangazwa katika mkutano huo pia.

Makampuni hasa ya teknolojia, kwa sasa yanaweza kuhamisha faida zao kwa urahisi katika nchi zilizo na viwango vya chini vya utozaji kodi, licha ya kuwa kiwango cha biashara cha makampuni hayo katika nchi hizo ni kidogo.

Ila kuna hofu pia kuhusiana na hatua ya nchi saba zilizostawi kiviwanda G7 kuvipa kipau mbele vita vya Urusi na Ukraine, ni jambo linaloweza kupelekea makubaliano ya mwisho kutofikiwa.

Vyanzi: AFP/Reuters