Ethiopia na Tigray wakubaliana kusitisha moja kwa moja vita
2 Novemba 2022Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ametoa tangazo hilo alipokuwa akiarifu kwa mara ya kwanza matokeo ya mazungumzo ya amani nchini Afrika Kusini na kuongeza kuwa serikali ya Ethiopia na mamlaka za jimbo la Tigray wameagiza upokonyaji wa kupangwa wa silaha na usio na vurugu. Makubaliano mengine ni pamoja na kurejeshwa kwa sheria na utulivu pamoja na huduma, lakini pia kuruhusu ufukishwaji wa huduma za kibinaadamu.
Soma Zaidi: Muungano wa Afrika waandaa mazungumzo ya amani Ethiopia
Amesema "Huu sio mwisho wa mchakato wa amani ndio kwanza tunauanza. Utekelezaji wa mkataba wa amani uliotiwa saini hii leo ni muhimu kwa mafanikio ya mchakato huu.”
Kiongozi wa ujumbe wa serikali ya Ethiopia kwenye mazungumzo hayo Redwan Hussein amesema ni wakati kwa pande hizo zote kuheshimu makubaliano, sawasawa na kiongozi wa upande wa Tigray Getachew Reda, ingawa alilisitiza kwamba makubaliano yaliyofikiwa si mepesi hata kidogo.
Vita baina ya mahasimu hao vinatimiza miaka miwili siku ya Ijumaa na vimesababisha mateso makubwa kwa raia na uharibifu wa hali ya juu, amesema Redwan.
Kuna wasiwasi iwapo Eritrea, mshirika wa Ethiopia ataheshimu makubaliano hayo.
Eritrea ambayo imekuwa ikiisaidia serikali ya Ethiopia pia ilishiriki mazungumzo hayo, ingawa haikujulikana mara moja ni kwa kiasi gani serikali yake ya kikandamizaji, ambayo kwa muda mrefu imewachukulia wanajeshi wa Tigray kama kitisho, itayaheshimu makubaliano hayo, alisema waziri wa habari wa Eritrea alipokuwa akijibu maswali.
Vikosi vya Eritrea vimekuwa vikilaumiwa kwa vitendo vya unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa makundi na baadhi ya mashuhuda wamesema waliowaona wanajeshi wa Eritrea wakiwaua na kupora mali za raia hata wakati mazungumzo hayo yakiendelea.
Jana Jumatano duru za misaada ya kibinaadamu zimesema wanawake kadhaa katika mji wa Adwa waliripotiwa kubakwa na wanajeshi wa Eritrea na miongoni mwao walijeruhiwa vibaya.
Vikosi kutoka jimbo la Amhara nchini Ethiopia pia vimekuwa vikipambana na wanajeshi wa Tigray, lakini hawakuwa na uwakilishi kwenye mazungumzo hayo ya amani. Mwenyekiti wa taasisi ya Amhara Association of America Tewodrose Tirfe amesema wanajeshi wake hawatarajii kukubaliana na matokeo yoyote ya mchakato huo ambao wanaona kama hawakujumuishwa.
Ulimwengu waikaribisha hatua hiyo chanya.
Ulimwengu umesifu mafanikio yaliyofikiwa kwenye mazungumzo hayo. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kupitia msemaji wake Stephane Dujarric ameyakaribisha matokeo hayo akisema ni hatua ya kwanza ya kumaliza mapigano na yatakayoleta matumaini kwa mamilioni ya watu wa Ethiopia walioteseka wakati wa mapigano. Umoja wa Ulaya, umezitolea mwito kama huo pande hizo mbili.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Ned Price amewaambia waandishi wa habari kwamba makubaliano hayo ni yanawakilisha hatua muhimu kuelekea amani, kusitishwa kwa uhasama pamoja na kuandaa mazingira ya kumaliza ukiukwaji wa haki za binaadamu na mauaji ya kiholela.
Soma Zaidi:Marekani kumtuma mjumbe maalum Ethiopia kutuliza vita
Rais wa Umoja wa Afrika Macky Sall amesema hizo ni taarifa njema mno na kuzipongeza pande hizo mbili, huku akiwahamasisha kufikia amani ya kudumu, huku rais wa Kenya William Rutto, naye akiyakaribisha matokeo hayo na kumpongeza waziri mkuu Abiy na uongozi wa Tigray, akiwasihi kuyetekeleza ili kufikia amani ya kudumu.
Suala kuu linalosalia kwa sasa ni juu ya muda gani hasa ambapo misaada itaanza kupelekwa tena Tigray, ambako huduma za mawasiliano na usafirishaji zimeharibiwa vibaya tangu mapigano yalipoanza. Madaktari wamesema wamepungukiwa dawa muhimu kama chanjo, dawa za kisukari na vyakula vya dawa, na watu wamekuwa wakifa kwa magonjwa yanayozuilika pamoja na njaa.
Mzozo kati ya serikali ya Ethiopia na Tigray ulianza Novemba 2020, chini ya mwaka mmoja tangu waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alipotunukiwa tuzo ya kimataifa ya amani ya Nobeli baada ya kufanikisha kupatikana kwa amani na Eritrea.
Mashirika:APE/RTRE/AFPE