Muungano wa Afrika waandaa mazungumzo ya amani Ethiopia
5 Oktoba 2022Serikali mjini Addis Ababa ilikiri kupokea mualiko huo, ikisema iko tayari kushiriki mkutano huo nchini Afrika Kusini, kwa mujibu wa mshauri wake wa masuala ya usalama, Redwan Hussein.
"Muungano wa Afrika imetowa mualiko wa mazungumzo ya amani. Serikali imeukubali kwani unakwendana na hoja yetu kuhusiana na suluhisho la amani kwa mzozo huu na haja ya kufanya mazungumzo bila masharti." Aliandika mshauri huyo kupitia mtandao wa Twitter.
Ingawa haikufafanuliwa zaidi, msimamo wa serikali ya Ethiopia ni kwamba majadiliano yoyote ya kusaka amani kwenye mkoa wake wa kaskazini wa Tigray lazima yasimamiwe na Muungano wa Afrika na kwamba pande zote zisiweke masharti yoyote kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo.
Kwa mujibu wa mwanadiplomasia mmoja wa Muungano wa Afrika, wawakilishi wa Muungano wa Ulaya na Umoja wa Mataifa pamoja na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano wa Pembe ya Afrika (IGAD) pia wanatazamiwa kuhudhuria mazungumzo hayo kama watazamaji.
Kuelekeo suluhisho la kudumu
Barua kutoka Kamisheni ya Muungano wa Afrika inasema mazungumzo hayo yanadhamiria "kuweka msingi wa majadiliano ya kina kati ya pande hizo mbili kuelekea suluhisho la kudumu la mzozo huo."
Barua hiyo iliyoonekana na mashirika ya habari inasema kuwa mjumbe maalum wa Muungano wa Afrika na rais wa zamani wa Nigeria, Olesegun Obasanjo akisaidiwa na rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta na aliyekuwa naibu rais wa Afrika Kusini, Phumzile Mlambo-Ngcuka, watasimamiia mazungumzo hayo.
Mwanadiplomasia mwengine kwenye makao makuu ya Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba bado wanangojea jibu kutoka upande wa Tigray. Msemaji wavikosi vya Tigray, Getachew Reda, hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hili.
Mkutano wa kwanza ngazi za juu
Ikiwa mkuu wa vikosi hivyo, Debretsion Gebremichael, atahudhuria mazungumzo hayo kati yao na serikali kuu ya Ethiopia, yatakuwa ya kwanza ya ngazi za juu kabisa katika jitihada za kukomesha miaka miwili ya vita vilivyokwishauwa maelfu ya watu kwa risasi na kwa njaa.
Mazungumzo haya yanakuja zaidi ya mwezi mmoja tangu mapigano yaanze upya baada miezi kadhaa ya utulivu.
Kwa mujibu wa TPLF, vikosi kutoka nchi jirani,Eritrea, vimeungana tena na jeshi la Ethiopia kushambulia maeneo yanayoshikiliwa na wapiganaji wa kundi la TPLF katika mkoa wa Tigray.
Mapigano hayo yamesambaa pia kwenye mikoa mingine ya Amara na Afar wakati wapiganaji wa TPLF wakijaribu kuishinikiza serikali kuu mjini Addis Ababa, huku Umoja wa Mataifa ukisema pande zote zimehusika na matukio ya uhalifu wa kivita.