1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eritrea yadaiwa kufanya mashambulizi ya mpakani

20 Septemba 2022

Msemaji wa mamlaka ya Tigray Getachew Reda, amesema Eritrea imefanya mashambulizi katika mpaka wa taifa hilo na kaskazini mwa Ethiopia katika kile kinachoonekana kuwa kuongezeka kwa mapigano yaliozuka mwezi uliopita.

https://p.dw.com/p/4H78n
Äthiopien I Konfliktregion Tigray
Picha: Ethiopian News Agency/AP/picture alliance

Reda amesema Waeritrea wanapigana pamoja na vikosi vya shirikisho la Ethiopia, ikiwa ni pamoja na vitengo vya makomando na wanamgambo washirika. Katika ujumbe kupitia mtandao wa twitter, Reda amesema kuwa Eritrea inapeleka jeshi lake lote pamoja na wanajeshi wa akiba na kwamba vikosi vyao vinatetea ngome zao kishujaa.

Kulingana na shirika la habari la AP, Mfanyakazi mmoja wa msaada anayefanya kazi Kaskazini mwa Ethiopia katika mji wa Adigrat, amesema kuwa vikosi vya Eritrea vinashambulia maeneo ya karibu. Waziri wa habari wa Eritrea Yemane Gebremeskel hakujibu mara moja ombi la tamko.

Iwapo itathibitishwa, mashambulizi hayo yataashiria kuongezeka kwa vita ambavyo tayari vimesababisha mamilioni ya watu kuyakimbia makazi yao na kusababisha maafa ya kibinadamu Kaskazini mwa Ethiopia.

Getachew amesema wanajeshi wa Ethiopia na vikosi maalum kutoka upande wa Kusini wa eneo la Amhara walikuwa wamejiunga katika mashambulizi hayo. Msemaji wa serikali ya Ethiopia Legesse Tulu, msemaji wa jeshi kanali Getnet Adane na msemaji wa waziri mkuu Billene Seyoum, hawakujibu mara moja kuhusu ombi la tamko. Gizachew Muluneh, msemaji wa serikali ya eneo la Amhara pia hakujibu mara moja ombi la tamko.

Äthiopien | Premierminister Abiy Ahmed Ali
Abiy Ahmed - Waziri mkuu wa EhtiopiaPicha: Office of the Prime Minister Ethiopia/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Uingereza na Canada zatoa ushauri wa kusafiri

Wiki iliyopita, Uingereza na Canada zilitoa ushauri wa kusafiri, zikiwataka raia wao nchini Eritrea kuwa waangalifu baada ya mamlaka katika eneo hilo kuwataka raia wake kuchukuwa majukumu ya kijeshi.

Vikosi vya Eritrea vilipigana katika upande wa wanajeshi wa shirikisho la Ethiopia huko Tigray wakati vita vilipoanza Novemba 2020. Vikosi vya Eritrea vilihusishwa katika ukatili mbaya zaidi uliofanywa katika mzozo huo, mashtaka wanayokanusha. Mapigano hayo yalizuka upya mnamo mwezi Agosti baada ya kutulia kwa vita hivyo mapema mwaka huu. Mzozo huo unakadiriwa kusababisha vifo vya maelfu ya watu na kuacha mamilioni bila huduma za msingi kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Ndani ya Tigray, mamilioni ya wakaazi bado wametengwa kwa sehemu kubwa na dunia. Huduma za benki na mawasiliano zimekatizwa na kurejeshwa kwa huduma hizo kumekuwa sharti kuu katika juhudi za upatanishi. Kuingia kikamilifu kwa Eritrea katika vita vya Tigray kunaonekana kutatiza juhudi zozote za amani kati ya viongozi wa Tigray na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ambaye alirekebisha uhusiano na Eritrea mara tu alipoingia madarakani mwaka 2018.