Eneo la mpakani kati ya Urusi na Ukraine laendelea kuwa tete
24 Mei 2023Gavana wa mkoa huo wa Belgorod, Vyacheslav Gladkov amearifu leo kuwa mashambulizi yameharibu majengo ya utawala, makaazi ya watu na magari, na kuongeza kuwa idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani, au droni zilizohusika imedunguliwa.
Soma zaidi: Mji wa Belgorod washambuliwa kwa ndege zisizo na rubani
Eneo hilo la magharibi mwa Urusi limekumbwa na hujuma kwa miezi kadhaa sasa, na Moscow inadai mawakala wa Ukraine wamekuwa wakiyafanya mashambulizi hayo kwa kutumia maguruneti na mizinga.
Ripoti ya Urusi imesema kuwa tangu Jumatatu, dazeni kadhaa za iliowaita ''wawakilishi wa vikosi vya jeshi la Ukraine'' wamekuwa wakiendesha operesheni katika mkoa huo. Hapo jana, jeshi la Urusi liliondoa hali ya dharura iliyokuwa imetangazwa katika eneo hilo, likisema lilichokitaja kuwa ni ''operesheni dhidi ya magaidi'' ilikuwa imemalizika.
Maandalizi ya uwanja wa mapigano
Ukraine imekanusha kuhusika katika hujuma hizo, ikisema badala yake kuwa operesheni hizo zinafanywa na wazalendo raia wa Urusi wanaopinga utawala wa rais Vladimir Putin.
Akizungumzia kinachoendelea katika eneo hilo la mpaka baina ya Urusi na Ukraine, mtaalamu wa masuala ya kijeshi aliyeko mjini London, Mark Galeotti amesema yumkini lengo lake ni kuandaa mazingira ya Ukraine kuanzisha harakati zake za kuyakomboa maeneo yanayokaliwa na Urusi.
Soma zaidi: Urusi yadai kuwasambaratisha wanamgambo waliovamia Belgorod
''Pengine hiki ni kile ambacho katika lugha ya kijeshi kinajulikana kama kuandaa mazingira kwenye uwanja wa mapambano, kwa ajili ya mashambulizi ya kulipa kisasi ya Ukraine ambayo hayaepukiki,'' amesema Galeotti na kuongeza kuwa ''lengo la kwanza ni kuitia wasiwasi Urusi juuya kuwepo kwa uasi wa ndani, na lengo la pili ni kuifanya Urusi iwatawanye wanajeshi wake, ikiwapeleka baadhi yao kutoa msaada katika mkoa wa Belgorod.''
Mbali na Ukraine, Urusi pia iliihusisha Marekani na matukio katika mkoa huo wa Belgorod, ikichapisha picha za zana za kijeshi zinazotengenezwa nchini Marekani iliyodai ziliharibiwa katika operesheni ya kupambana na wavamizi. Marekani imezipinga tuhuma hizo.
Kiongozi wa kundi la Wagner aonya kuwa Urusi inabweteka
Huku hayo yakijiri, kamanda wa kundi binafsi la wapiganaji la nchini Urusi la Wagner, Yevgen Prigozhin ameonya juu ya uwezekano wa Urusi kukumbwa na vuguvugu la mapinduzi mithili ya lile la mwaka 1917, na kwamba hali hiyo inaweza kuisababishia nchi hiyo kuvipoteza vita vyake dhidi ya Ukraine.
Soma zaidi:Urusi yadai Ukraine imehusika kushambulia eneo lake la mpakani la Belgorod
Prigozhin amesema njia pekee ya kuiepusha hali hiyo ni ikiwa kundi la watu wenye ushawishi nchini Urusi litaacha mzaha katika kupigana vita hivyo. Amesema kuna dhana nchini Urusi kuwa nchi za magharibi zitachoka na vita, na kwamba China itafanikiwa kuusuluhisha mgogoro huu, na kuongeza kuwa binafsi anaamini kuwa dhana hiyo haina mashiko.
Vyanzo: dpae,rtre