1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yadai kuwasambaratisha wanamgambo waliovamia Belgorod

23 Mei 2023

Urusi imesema imepeleka ndege za kivita na mizinga kwa ajili ya kulisambaratisha kundi lenye silaha lililojipenyeza kwenye mpaka wake kutoka Ukraine, huku Ikulu ya Kremlin ikitaka jeshi kuzuia mashambulizi mengine zaidi.

https://p.dw.com/p/4RiOC
Ukraine Charkiw | beschädigtes Verkehrsschild, Richtung Belgorod
Picha: Vadim Ghirda/AP Photo/picture alliance

Mapigano hayo ni mabaya zaidi kushuhudiwa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwaka uliopita, hatua iliyoifanya Kremlin kuelezea wasiwasi wake mkubwa na kuwaondoa watu katika vijiji tisa vya jimbo la kusini la Belgorod.

Vikosi vya kitaifa vyasambaratishwa

Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Urusi iliyotolewa Jumanne imeeleza kuwa wakati wa operesheni ya kupambana na ugaidi, vikosi vya kitaifa vilizuiwa na kusambaratishwa na mashambulizi ya anga na mizinga.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, wapiganaji waliosalia walirudishwa katika eneo la Ukraine, ambako waliendelea kushambuliwa hadi walipoangamizwa kabisa. Urusi imesema imewaua zaidi ya wapiganaji 70 wa Ukraine na kuharibu magari manne ya kivita.

Russland l Gouverneur der Region Belgorod - Wjatscheslaw Gladkow
Gavana wa Belgorod, Vyacheslav GladkovPicha: Sputnik/Mikhail Klimentyev/Kremlin via REUTERS

Gavana wa Belgorod, Vyacheslav Gladkov amesema raia wameondolewa kwenye vijiji tisa katika jimbo hilo, ambalo awali lilikabiliwa na mshambulizi ya makombora ambayo yaliwaua watu kadhaa, tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

"Tunaendelea kuwasihi wakaazi walioondolewa kwenye nyumba zao kwa sasa wasirejee nyumbani. Tutawajulisha haraka kupitia mitandao ya kijamii, na wakuu wa serikali za mitaa watawapa taarifa, hali itakapokuwa salama," alifafanua Gladkov.

Mwanamke mmoja afariki wakati wa kuondolewa

Gladkov amesema kwa bahati mbaya mwanamke mmoja aliyezaliwa mwaka 1941, alifariki wakati wa shughuli ya kuwaondoa watu, na wakaazi wamepelekwa kwenye makaazi ya muda huko Stary Oskol.

Wapiganaji wa kikosi kinachopinga Uhuru wa Jeshi la Urusi, kimedai kuhusika na uvamizi wa Belgorod, huku Ukraine ikikanusha kuhusika. Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Ganna Malyar amesema hawapigani vita kwenye maeneo ya kigeni.

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema kuna uwezekano mkubwa kwamba vikosi vya usalama vya Urusi vilipambana na wapiganaji katika maeneo takribani matatu kwenye jimbo la Belgorod. Mshauri wa rais wa Ukraine, Mikhaylo Podolyak amesema kuwa makundi ya wapiganaji wa msituni ya Urusi huenda yanahusika na mashambulizi hayo.

Russland-Ukraine-Krieg | Kämpfe in Belgorod
Watu wakiliangalia jengo ambalo limeshambuliwa BelgorodPicha: AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo, rais wa zamani wa Urusi, Dmitry Medvedev ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Usalama lenye nguvu la Rais wa Urusi, Vladmir Putin ameonya kuwa kadri nchi za Magharibi zinavyoipatia Ukraine silaha zaidi za maangamizi, ndivyo hatari ya vita vya nyuklia inavyoongezeka.

Msaada zaidi kwa Ukraine

Ama kwa upande mwingine mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema nchi za umoja huo zimetoa risasi 220,000 kwa ajili ya mifumo ya kurushia makombora, pamoja na makombora 1,300 kwa Ukraine, chini ya mpango uliokubaliwa na mawaziri mwezi Machi.

Aidha, akizungumza Jumanne mjini Brussels, Ubelgiji kwenye mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya, Borrell amesema mafunzo ya marubani wa Ukraine kwa ajili ya kurusha ndege za kivita chapa F-16 yameanza nchini Poland, baada ya Marekani kutoa idhini.

(AP, AFP, Reuters)