1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eid al-Adha: Viongozi Tanzania wahimiza umoja na amani

17 Juni 2024

Viongozi wa serikali nchini Tanzania wametumia sikukuu ya Eid kuzungumzia masuala mbalimbali ya kitaifa na kuhimiza umoja na amani na uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4h8aL
Muumini wa Kiislamu akiwema sawa kilemba chake wakati wa sala ya Eid al-adha
Muumini wa Kiislamu akiwema sawa kilemba chake wakati wa sala ya Eid al-adhaPicha: AFP

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyeongoza baraza la Eid lililofanyika jijini Dar es salaam amewataka waumini wa dini ya kiislamu kuzingatia misingi dini kwa kutenda mema na kutumia siku ya  leo kuwafikia wale wenye mahitaji kwa kuwapa misaada ya hali na mali.

Ama kuhusu masuala ye kitaifa, waziri mkuu amewakumbusha wananchi kuhusu umuhimu wa kuendelea kulinda mazingira akionya janga linaloweza kulikumba taifa iwapo suala hilo litapuuzwa.

Amesema tayari serikali imeanza kuchukua hatua ya kuyahami mazingira ikiwamo kuendesha kampeni ya kimataifa yenye shabahab ya kuhamasisha umma kuhusu ulinzi mazingira akitolea mfano namna Rais Samia Suluhu Hassan alivyoshiriki katika mikutano ya kimataifa yenye ajenda ya kukusanya mafungu ya fedha kugharimia miradi ya ulinzi wa mazingira.

Soma pia:Waumini wa Kiislamu wakusanyika kwa ajili ya ibada katika mlima Arafat

Kuhusu uchaguzi wa serikali wa mitaa utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu, kiongozi huyo amewakumbusha wananchi namna wanavyopaswa kuanza kijiandaa na uchaguzi huo na kwamba wanapaswa kutambua haki walizo nazo za kuchagua na kuchaguliwa.

Hadi sasa tume huru ya taifa ya uchaguzi haijatangaza ni lini uchaguzi huo utafanyika lakini inakusudia kufanya hivyo mnamo mwezi Novemba.

Serikali Zanzibar kuweka mazingira rafiki kwa mahujaji

Naye Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyiametumia sherehe za sikuu ya ied kufahamisha namna serikali yake ilivyokusudia kuwawezesha wananchi wengi kwenda mahujai Saudia.

Rais Mwinyi aliyekuwa akizungumza katika baraza la Eid amesema kuna uwezekano mkubwa kuanzia mwakani shirika la ndege la saudia arabia likaanza kufanya safari za ndege moja kwa moja visiwani humu hatua ambayo itarahisisha wale wanakusudia kwenda kutekeleza ibada hiyo muhimu ya hija.

Waaumini wa dini ya kiislam Tanzania leo wanaungana na wengine duniani kusherekea sikuu ya eid al- Adha sherehe ambayo inahitimisha shughukli ya Hijja ikiwa ni moja ya Nguzo Tano za Uislamu.

Waislamu wote wanatakiwa kufanya ibada hiyo ya siku tano angalau mara moja katika maisha yao ikiwa wana uwezo wa kimwili na wa kifedha.

Baadhi ya waislamu waswali sala ya Eid Tanzania

Soma pia:Mahujaji wa Kiislamu wajiandaa kwa ibada rasmi ya Hija

Waislamu kutoka kote duniani walianza kukusanyika tangu Jumamosi katika viwanja vya mlima Arafat kwa ibaada maalumu. Inaaminika Mtume Muhammad SAW alitoa hotuba yake ya mwisho, inayojulikana kama hotuba ya kuaga katika mlima huo mtakatifu zaidi ya miaka 1,400 iliyopita.

Katika khutba hiyo, mtume alitoa wito wa kuwepo usawa na umoja miongoni mwa Waislamu. Na waumini wa dini ya Kiislamu waliokwenda katika hija hiyo wanatarajia kuanza kurejea nyumbani wiki hii.