1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wadau wa siasa walalamikia sheria za uchaguzi za Tanzania

10 Juni 2024

Wadau wa siasa nchini Tanzania bado wanalalamikia mapungufu yaliyojitokeza katika sheria za uchaguzi zilizopitishwa hivi karibuni na bunge la taifa hilo la Afrika Mashariki.

https://p.dw.com/p/4gsLa
Tansania | Uchaguzi wa Rais | 
Wadau wa siasa nchini Tanzania wamesema wanaishinikiza serikali kufanyia marekebisho baadhi ya sheria za uchaguziPicha: Ericky Boniphace/DW

Wadau hao pamoja na mambo mengine wameisisitiza serikali ya nchi hiyo kuwa na uchaguzi mmoja, utakaojumuisha serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

Wadau  wa siasa wakiongozwa na Jukwaa la Katiba Tanzania,JUKATA wamesema hayo Jumatatu walipokutana na wanahabari jijini Dar es Salaam,  na kubainisha kuwa, wanaishinikiza serikali ifanye mabadiliko ya katiba kwani kufanya chaguzi mbili tofauti, wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu, mwaka 2025, ni kuingia gharama zisizo na msingi.

Bob Chacha Wangwe, Mkurugenzi Mtendaji wa JUKATA ameiambia DW kuwa pamoja na serikali kuonyesha utashi wa kiasiasa na kufanya mabadiliko ya sheria, lakini bado kuna mapengo yanayochagiza uminywaji wa demokrasia.

Soma pia:CHADEMA yazinduwa 'Operesheni 255' kudai katiba mpya

"Sisi hatujaona sababu yoyote ya kimsingi ya kuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ambayo yanagharimu fedha na muda."

Tanzania, Dar es Salaam |
Wadau mbalimbali wamekuwa wakipaza sauti zao kutaka katiba mpya nchini Tanzania pamoja na marekebisho ya sheria za uchaguziPicha: Eric Boniface/DW

Amesema JUKATA  inaendelea kuzichambua sheria hizi licha ya kuwa zimeshapitishwa na bunge na kuongeza kuwa matokeo ya uchambuzi huo yanalenga kuendelea kuishinikiza serikali kuwajibika na kufanya maboresho ya sheria hizo.

Soma pia: Hisia za vyama vya siasa Tanzania kuhusu demokrasia ya nchi

Mwezi Februari mwaka huu, Bunge la Tanzania, lilipitisha miswada mitatu ya sheria za uchaguzi, Muswada wa sheria ya tume ya taifa ya uchaguzi, muswada wa sheria ya uchaguzi wa  rais, wabunge na madiwani na muswada wa sheria za marekebisho ya vyama vya siasa.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Ananilea Nkya amebainisha matokeo ya ripoti ya uchambuzi wao na akashauri zaidi kuhusu kuwa na chaguzi mbili au moja.

"Tumesema tunaendeleza kushinikiza serikali itambue jambo hili na vinavyotakiwa kufanyiwa marekebisho vifanyiwe."

Juni 9, chama cha wananchi CUF kilitangaza kufanya mazungumzo na vyama vingine vya siasa ili kuungana na kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi kwani sheria mpya zilizopitishwa februari mwaka huu ni danganya toto na maoni ya wadau walio wengi yalipuuzwa.

Sikiliza pia:

Maoni: Tanzania na Katiba mpya