1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kuitambua miili ya wanafunzi wa Endarasha kwa DNA

9 Septemba 2024

Uchunguzi wa kutumia vinasaba, DNA unatarajiwa kuanza leo nchini Kenya kusaidia kuwatambua wanafunzi waliopoteza maisha katika mkasa wa moto kwenye shule ya Hillside Endarasha katika kaunti ya Nyeri, wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/4kQEC
Maafisa kutoka ofisi ya mtaalamu wa upasuaji maiti wa serikali ya Kenya wakibeba miili ya wanafunzi waliofariki dunia katika shule ya msingi ya Hillside Endarasha katika kaunti ya Nyeri nchini Kenya mnamo Septemba 7,2024
Maafisa kutoka ofisi ya mtaalamu wa upasuaji maiti wa serikali ya Kenya wakibeba miili ya wanafunzi waliofariki dunia katika shule ya msingi ya Hillside EndarashaPicha: Edwin Walta/REUTERS

Watoto hao walifariki dunia siku ya Alhamisi baada ya moto kuteketeza bweni lao katika shule hiyo ya Hillside Endarasha walipokuwa wamelala.

Siku ya Jumamosi, msemaji wa serikali Isaac Mwaura, alisema miili 19 ilipatikana kwenye magofu yaliyoteketea ya jengo hilo, huku wanafunzi wengine wawili wakifia hospitalini, na 17 bado hawajulikani waliko.

Soma pia:Wanafunzi 17 wafariki kwa kuteketea moto Kenya

Polisi imesema miili ya wanafunzi hao, wenye umri wa kati ya miaka 9 na 13, iliteketea kiasi cha kutotambulika, na familia zimekuwa na wakati mgumu kusubiri kujua hatma ya wapendwa wao.

Hapo jana, kamishna wa kaunti ya Nyeri Pius Murigu, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba shughuli ya kitaalamu ya kufanyia uchunguzi miili hiyo itaanza leo kwa sababu hiyo ndio njia ya pekee miili hiyo inaweza kutambuliwa.

Familia za waathiriwa zahimizwa kujitokeza kutambua miili

Murigu alizihimiza familia zilizoathirika kujitokeza leo katika hospitali ya Naromoru na kushiriki katika mchakato unaofuata wa utambuzi huo wa kitaalamu wa mabaki ya miili ya wanafunzi hao kutokana na janga hilo.

Kwa upande wake, Johansen Oduor, mtaalamu mkuu wa upasuaji maiti wa serikali amesema walifanikiwa kuipata miili 19 ambayo imeungua sana kiasi kwamba isingewezekana kwa wazaziwao kuweza kuitambua.

Hata hivyo, Oduor amesema upasuaji wa maiti kwa uchunguzi utaanza kesho Jumanne.

Wazazi na jamaa za wanafunzi wa shule ya msingi ya Hillside Endarasha wakusanyika shuleni humo baada ya moto kuzuka na kusababisha vifo vya wanafunzi kadhaa mnamo Septemba 5.
Wazazi na jamaa za wanafunzi wa shule ya msingi ya Hillside Endarasha wakusanyika shuleni humo baada ya kuzuka kwa motoPicha: Simon Maina/AFP

Siku ya Ijumaa Rais William Ruto aliagiza kufanywa kwa uchunguzi kamili juu ya mkasa huo.

Soma pia:Moto shuleni: Rais Ruto atangaza maombolezo ya siku tatu

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limekuwa likitoa ushauri wa kisaikolojia kwa watoto na jamaa waliopatwa na kiwewe, huku wakiweka mahema meupe nje ya lango la shule hiyo ya Endarasha.

Usalama wa shule nchini Kenya watiliwa shaka

Tukio hilo la Alhamisi limeangazia suala la usalama katika shule nchini Kenya, baada ya kutokea visa vingi sawa na hicho katika miaka ya nyuma vingi vikiwa vibaya mno.

Huku hayo yakijiri, siku ya Jumamosi usiku moto mwingine ulizuka katika shule ya sekondari ya wasichana ya Isiolo pia katika eneo la Kati mwa Kenya huku picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha majengo mengi yakiteketea.

Soma pia:Makamu wa Rais Kenya asema wanafunzi 70 hawajulikani walipo baada ya ajali ya moto

Mkurugenzi wa mawasiliano katika kaunti ya Isiolo Hussein Salesa, ameiambia AFP kwamba kulikuwa na majeruhi kadhaa, lakini polisi inasema hakuna aliyejeruhiwa.

Hapo jana Jumapili, moto mwingine uliteketeza bweni katika shule ya sekondari ya wavulana ya Njia katika kaunti ya Meru wakati wanafunzi walipokuwa wakila chakula cha jioni. Haya ni kulingana na taarifa ya polisi. Hata hivyo, hakuna majeruhi walioripotiwa.