1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Conservative wasaka uongozi mpya

1 Oktoba 2024

Wagombea wanne wanaowania uongozi wa chama cha Conservative nchini Uingereza, walianza kuelezea maono yao kwa taifa siku ya Jumapili, huku uhamiaji likiwa suala kubwa katika mijadala ya mustakabali wa chama hicho.

https://p.dw.com/p/4lHMG
Uingereza London | Rishi Sunak
Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na kiongozi anayemaliza wake wa chama cha Conservative, Rishi Sunak.Picha: Tayfun Salci/ZUMA Press/picture alliance

Mwanzoni mwa mkutano wa mwaka wa chama hicho mjini Birmingham, wagombea hao wanne, wanaowajumuisha waziri wa zamani wa uhamiaji Robert Jenrick na mwenzake wa biashara, Kemi Badenoch, waliwasilisha azma yao ya kutaka nafasi ya kiongozi mpya wa chama hicho .

Baada yake miaka 14 madarakani kumalizwa kwa ushindi mkubwa wa chama cha Labour mwezi Julai, wafuasi wa Conservative wameanza kujitafajkari huku wengi wakisema kiongozi mpya lazima akabiliane na kumaliza migogoro ya ndani na ukosefu wa utendajikazi bora, mambo wanayoamini kuwa yalichangia chama hicho kupata matokeo mabaya zaidi ya uchaguzi katika historia yake ndefu.

Soma zaidi: UK yatumia fedha za mpango wa uhamishaji waomba hifadhi Rwanda kuimarisha usalama mpakani

Waziri mkuu wa zamani, Rishi Sunak, anayeachia madaraka, alihutubia mkutano huo kwa ufupi na kusema hatatoa hotuba ya kawaida ya kiongozi ili kuruhusu wagombea hao wanne kujinadi mbele ya chama hicho.

Sunak alitoa wito kwa chama hicho kushirikiana na kiongozi atakayechaguliwa.

Robert Jenrick, mgombea uongozi wa Conservative.
Robert Jenrick, mgombea uongozi wa Conservative.Picha: Yui Mok/empics/picture alliance

Wagombea wakuu, Jenrick na Badenoch, waliangazia zaidi suala la uhamiaji, huku wote wakisema serikali zilizotangulia za chama cha Conservative zilishindwa pakubwa kushughulikia suala hilo ambalo wapiga kura wanasema linazidi kuathiri utoaji wa huduma za umma ambazo tayari zinalemewa kama vile afya.

Mkataba wa Haki za Kibinaadamu

Jenrick aliiambia televisheni ya Sky News kwamba ataweka mpango utakaoilazimisha Uingereza kuruhusu idadi fulani ya  wahamiaji kuingia nchini Uingereza na kuongeza kuwa nchi hiyo inapaswa kujiondoa katika Mkataba wa Haki za Kibinadamu wa Ulaya, ambao uliidhinishwa  na karibu mataifa yote ya Ulaya.

Kemi Badenoch
Kemi Badenoch, mgombea uongozi wa chama cha Conservative.Picha: Tayfun Salci/ZUMA/picture alliance

Mkataba huo hata hivyo unapingwa na baadhi ya wafuasi wa kihafidhina wakiukosoa kwa kusababisha kusitishwa kwa safari za ndege za kuwahamisha waomba hifadhi.

Soma zaidi: Mpango tata wa kupunguza ruzuku Uingereza wapitishwa na bunge

Badenoch alijibu kwa kusema ingawa idadi ni muhimu, suala la ushirikiano na utamaduni ni muhimu zaidi . 

Badenoch ameiambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa anayeingia nchini humo ni muhimu kabisa, na uongozi unahitaji kuanza kutoka juu.

Wagombea wote wanne, akiwemo waziri wa zamani wa mambo ya nje, James Cleverly, na mwenzake wa usalama, Tom Tugendhat, walisema chama cha Conservative kinahitaji kurejesha imani ya wapiga kura baada ya kuipoteza katika miaka kadhaa ya mivutano ya ndani pamoja na kashfa.

James Cleverly
James Cleverly, mgombea uongozi wa chama cha Conservative.Picha: Toby Melville/REUTERS

Soma zaidi: Keir Starmer aanza kazi rasmi hii leo

Kiongozi huyo mpya atakuwa wa tano wa chama hicho tangu waziri mkuu wa zamani, David Cameron, kujiuzulu mnamo mwaka 2016.

Kongamano la kila mwaka la chama cha Conservative linagubikwa na suala la kinyang'anyiro cha nafasi ya uongozi wa chama hicho, huku wagombea wote wanne wakitarajiwa kuwahutubia wajumbe siku ya Jumatano (Oktoba 2) kabla ya kufanyika mchujo utakaowaacha wagombea wawili.

Baada ya hapo, wajumbe watapiga kura zao kumchagua kiongozi mpya atakayetangazwa Novemba 2.