1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango tata wa kupunguza ruzuku Uingereza wapitishwa

11 Septemba 2024

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amevuka kihunzi cha kwanza cha uongozi wake baada ya wabunge kuunga mkono mpango tata wa serikali yake wa kufuta ruzuku ya mafuta kwa kundi kubwa la wastaafu wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4kU3B
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer.Picha: Simon Dawson/Avalon/Photoshot/picture alliance

Mapendekezo hayo yamezusha hasira miongoni mwa wabunge wa chama tawala cha Labour na msuguano wa kwanza na vyama vya wafanyakazi wanaoiunga mkono serikali ya Starmer tangu alipoingia madarakani mwezi Julai.

Mgawanyiko huyo umedhihirisha kuwa changamoto kubwa kwa kiongozi huyo wa siasa za wastani za mrengo wa shoto ambaye anajaribu kurekebisha uchumi anaosema uliharibiwa na serikali iliyotangulia ya chama cha Conservative huku akilenga kutowaghadhibisha wale wanaomuunga mkono.

Mwenyewe amekiri kwamba mpango huo wa kuondoa ruzuku ya mafuta kwa wastaafu haukubaliki na wengi lakini amesisitiza ni muhimu katika kupunguza nakisi ya kiasi dola bilioni 29 kwenye bajeti ya taifa anayosema iliachwa na serikali iliyopita.