1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UK: Fedha za mpango wa Rwanda kuimarisha usalama mpakani

17 Septemba 2024

Karibu dola milioni 100 zilizotengwa na serikali ya Uingereza kuwahamisha waomba hifadhi nchini Rwanda zitatumiwa sasa kulipia teknolojia mpya na watumishi kukabiliana na magenge ya kusafirisha watu.

https://p.dw.com/p/4kiS0
Frankreich-UK Migration | Vorfälle beim Überqueren des Ärmelkanals
Picha: Gareth Fuller/empics/picture alliance

Wirara ya Mambo ya ndani ya Uingereza imesema dola milioni 100 zilizotengwa na serikali iliyopita ya Uingereza kwa ajili ya kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda sasa zitatumika kulipia teknolojia mpya na wafanyakazi wa kukabiliana na magenge yanayosafirisha watu.

Serikali mpya inayoongozwa na chama cha Labour iliyochaguliwa kwa kishindo mnamo Julai, iliutupilia mbali mpango tata wa serikali iliyopita ya chama cha Conservatives iliyokuwa chini ya Rishi Sunak na kuuita ni ufujaji wa pesa za walipa kodi.

Badala yake,Serikali ya waziri mkuu Keir Starmer imekuja na mpango wa kuvunja magenge ambayo yanafaidika kutoka kwa wahamiaji wanaotaka kuvuka kuingia nchini humo kutoka kaskazini mwa Ufaransa.

Soma pia: Sunak akwama tena bungeni kupeleka wakimbizi Rwanda

Haya yanajiri baada ya zaidi ya wahamiaji 1,000 kuwasili nchini Uingereza mwishoni mwa juma lililopita ambapo watu wanane walikufa wakati meli yao iliyokuwa imejaa watu wengi ilipozama katika pwani ya Ufaransa.

Meli hiyo ilikuwa ikijaribu kuvuka njia ya meli ambayo mara zote imekuwa yenye shughuli nyingi. Tukio hilo la wiki ya jana limejiri wiki mbili baada ya watu wengine 12 kupoteza maisha katika jaribio kama hilo.

UK | Waziri wa mambo ya ndani | Yvette Cooper
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper.Picha: Lucy North/PA Wire/dpa/picture alliance

Matumizi ya teknolojia kuzuwia walanguzi

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Yvette Cooper amesema pauni milioni 75 sawa na dola milioni 99 ambazo zilikuwa zitumike katika mpango wa Rwanda wa kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda sasa zitawekezwa katika vifaa vya uchunguzi wa siri ili kuongeza ukusanyaji wa ushahidi kwa ajili ya kuwafungulia mashtaka viongozi wa magenge.

Pesa hizo pia zitatumika kuwafadhili wafanyikazi zaidi wa usalama katika maeneo ya mpakani na wachunguzi zaidi 100 waliobobea katika Shirika la Kitaifa la Uhalifu, kama sehemu ya mbinu iliyojumuishwa zaidi kati ya utekelezaji wa sheria kushughulikia suala hilo.

Soma pia:Chama cha Labour chaahidi neema Uingereza 

"Tutatumia teknolojia ya hali ya juu na uwezo ulioimarishwa wa kijasusi ili kuhakikisha kuwa tunakomesha biashara hii mbaya", alisema Cooper katika taarifa yake.

Serikali ya Uingereza inasema inataka kukabiliana na tatizo hilo kwa kushirikiana na majirani zake wa karibu katika bara la Ulaya kuzuia wahamiaji zaidi ambao wanahatarisha maisha yao kwa kutaka kuvuka bahari.

Ruanda Kigali | Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Priti Patel asaini makubaliano kuhusu wakimbizi na waziri wa mambo ya nje Vincent Birutaare
Aliekuwa waziri wa mambo ya ndani katika serikali ya kihafidhina ya waziri mkuu Rishi Sunak, Priti Patel, na waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Biruta baada ya kusaini mpango wa kuhamisha waomba hifadhi nchini Rwanda, Aprili 14, 2022. Picha: Simon Wohlfahrt/AFP/Getty Images

Tayari imeongeza idadi ya maafisa wa Uingereza walioko Europol ambao ni mawakala wanaosimamia utekelezaji wa sheria za Umoja wa Ulaya ili kusaidia juhudi za Ulaya katika kuvunja mtandao wa kusafirisha watu.

Soma pia: Bunge la Uingereza laridhia kupeleka wakimbizi Rwanda

Waziri Mkuu Kier Starmer alikuwa mjini Roma hapo jana kujadili za Italia za kupunguza uhamiaji usio wa kawaida, ikiwa ni pamoja na mipango ya kuendesha vituo vya wahamiaji vinavyoendeshwa na Italia nchini Albania.

Mwezi Julai Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Cooper aliuita mpango wa Conservatives' wa Rwanda kuwa ni ''ufujaji''wa kushangaza zaidi wa pesa za walipa kodi ambao amewahi kuona.

Cooper aliliambia bunge kuwa pauni milioni 700 tayari zilitumika katika mpango huo wa kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda na serikali ilikuwa imepanga kutumia zaidi ya pauni bilioni 10 kwa jumla.