China na Afrika Kusini zakubaliana kushirikiana zaidi
3 Septemba 2024Rais Xi Jinping wa China na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini walikutana jana Jumatatu kabla ya kongamano la tisa la ushirikiano wa China-Afrika. Pande hizo mbili ziliita ziara hiyo ya Ramaphosa kuwa ni yenye umuhimu mkubwa kuelekea maendeleo baina ya mataifa hayo.
Ramaphosa alimueleza Rais Xi kwamba alikuwa ananuia kupunguza pengo la kibiashara na China na kupitia upya muundo wa biashara baina ya Afrika Kusini na China, na kwa upande mwingine akitoa wito wa uzalishaji endelevu na uwekezaji utakaoibua nafasi za ajira.
Soma zaidi:Kongamano la China- Afrika kuja na matokeo yenye tija?
Kwa upande wake mwanadiplomasia wa ngazi za juu anayeshughulikia masuala ya Afrika nchini China amesema hii leo kwamba China na Afrika zitashirikiana kwa karibu katika kulinda maslahi ya mataifa yanayoendelea, katikati ya ongezeko la uhasama na fikra za Vita Baridi.
China yasema inanuia kuisaidia Afrika katikati ya misukosuko ya ulimwengu
Liu Yuxi amesema hayo kwenye mkutano wa waandishi wa habari kabla ya Mkutano wa Kilele wa mwaka huu wa China Afrika, unaofunguliwa rasmi kesho na kukutanisha viongozi wakuu na wawakilishi wa mataifa hayo ama FOCAC.
"Katika kukabiliana na kuongezeka kwa uhasama na fikra ya Vita Baridi, China na Afrika zitashirikiana kwa karibu ili kuimarisha ushirikiano wetu. Tutasaidiana zaidi katika masuala yanayohusu maslahi yetu ya msingi na kufanya kazi bega kwa bega ili kulinda maslahi ya nchi zinazoendelea."
Viongozi wa mataifa ya Afrika, tayari wameanza kuwasili mjini Beijing ambako kongamano hilo linafanyika. Rais Xi Jinping atalifungua na kuongoza kuanzia kesho Jumatano Septemba 4, hadi 6.
Viongozi watua Beijing kwa ajili ya FOCAC
Miongoni mwa marais ambao tayari wako Beijing na William Ruto wa Kenya. Hadi mwaka 2023, ukubwa wa biashara kati ya mataifa hayo mawili imefikia dola bilioni 8.106. Kenya hata hivyo ni moja ya mataifa ya Afrika yenye mzigo mkubwa wa madeni kutoka China, sambamba na Angola, Ethiopia, Misri na Nigeria.
Mataifa haya yamekuwa yakipewa mikopo kwa ajili ya kuendeleza miradi mikubwa ikiwa ni pamoja na mradi tata wa reli wa nchini Kenya wa thamani ya dola bilioni 5 na unaounganisha mji mkuu Nairobi na Mombasa. Lakini wakosoaji wanaikosoa Beijing kwa kuilemaza Afrika kwa madeni na kufadhili miradi ya miundombinu inayoharibu mazingira.
Marais wengine waliofika Beijing ni Samia Suluhu Hassan wa Tanzania. China na Tanzania wamekuwa na mahusiano na ni washirika wa kuaminiana wa muda mrefu na ambao wanasaidiana katika masuala yanayohusisha maslahi makubwa ya kila nchi. China na Tanzania pia walianzisha mpango madhubuti wa kimkakati wa ushirikiano mnamo mwaka 2022.
Marais wengine ni wa Namibia Nangolo Mbumba, Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felipe Nyusi wa Msumbiji, Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio, na wengineo.