1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiAsia

Utafiti: China yaongeza utoaji wake mikopo kwa Afrika

30 Agosti 2024

Wakopeshaji wa China waliidhinisha mikopo yenye thamani ya dola bilioni 4.61 kwa Afrika mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la kwanza la kila mwaka tangu mwaka 2016. Haya ni kulingana na utafiti wa chuo kikuu cha Boston.

https://p.dw.com/p/4k5J7
Afrina  | China | Rais Xi Jinping
Rais wa China Xi JinpingPicha: GIANLUIGI GUERCIA/Pool via REUTERS

Afrika ilipata mikopo ya zaidi ya dola bilioni 10 kwa mwaka kutoka China kati ya mwaka 2012-2018, kutokana na mradi mkubwa wa Rais wa nchi hiyo Xi Jinping wa ujenzi wa miundombinu na barabara (BRI), lakini ukopeshaji huo ulipungua kwa kiasi kikubwa tangu kuanza kwa janga la UVIKO-19 mnamo mwaka 2020.

Kiwango cha mwaka jana, ambacho ni ongezeko la zaidi ya mara tatu kutoka mwaka 2022, kinaonesha kuwa China iko makini kukabiliana na athari zinazohusiana na mataifa yenye madeni makubwa .

Kituo hicho cha sera ambacho kinasimamia mradi wa kanzudata ya mikopo ya China kwa Afrika, kimesema inaonekana China inajaribu kutafuta kiwango endelevu cha usawa cha ukopeshaji na kufanya majaribio ya mkakati mpya.

Soma pia:Ghana yapata makubaliano ya kuangalia upya deni lake

Mikopo mikubwa zaidi ya mwaka jana ni pamoja na mkopo wa karibu dola bilioni 1 kutoka Benki ya Maendeleo ya China kwa Nigeria kufadhili mradi wa ujenzi wa reli kutoka Kaduna hadi Kano na kiwango sawa na hicho cha mkopo kwa Benki kuu ya Misri.

China imejivunia kuwa mkopeshaji mkuu kwa mataifa mengi kama vile Ethiopia katika miaka ya hivi karibuni.

Deni la Afrika kwa China linaongezeka

Utafiti huo wa chuo kikuu cha Boston pia umegundua kuwa China imelikopesha bara Afrika jumla ya dola bilioni 182.28 kati ya mwaka 2000-2023, huku kiwango kikubwa cha fedha kikitumika katika sekta za nishati, usafiri na teknologia ya habari na mwasiliano barani Afrika.

Afrika ilikuwa mstari wa mbele katika miaka ya mwanzo ya BRI, wakati China ilipojaribu kupanua ushawishi wake wa kijiografia na kiuchumi kupitia ufadhili wa ujenzi wa miundombinu ya kimataifa.

Je, China yaendeleza ukoloni mamboleo Afrika?

Soma pia:Mikopo inayohusishwa na maliasili za Afrika yakosolewa

Hata hivyo China, ilianza kupunguza mikopo hiyo mwaka 2019, mabadiliko ambayo yalichochewa na janga hilo la UVIKO-19 na miradi mingi ikakosa kukamilika katika eneo hilo lote, ikiwemo reli ya kisasa iliyokusudiwa kuiunganisha Kenya na majirani zake.

Kupungua kwa mikopo hiyo, kulisababishwa na mashinikizo ya ndani ya China na kuongezeka kwa mizigo ya madeni miongoni mwa mataifa ya Afrika.

Zambia, Ghana na Ethiopia zimeingia kwenye mpangilio mpya wa madeni ya muda mrefu tangu 2021.

Mkakati kujiondoa kwenye madeni

Utafiti huo pia umegundua kwamba zaidi ya nusu ya mikopo iliyotolewa mwaka jana, ama dola bilioni 2.59 zilikuwa za wakopeshaji wa kikanda na kitaifa, na kutilia mkazo mkakati mpya wa China .

Utafiti huo pia umeonesha kuwa hatua ya wakopeshaji wa China kuziangazia taasisi za kifedha za Afrika ina uwezekano mkubwa kwamba inawakilisha mkakati wa kupunguza hatari ya kujiingiza katika changamozo za madeni za mataifa ya Afrika.

Soma pia:China au Marekani: Nani anachelewesha msamaha wa madeni kwa mataifa maskini?

Tanzania na China zasaini hati 15 za makubaliano

Takriban moja ya kumi ya mikopo ya mwaka 2023 ilikuwa ya miradi mitatu ya nishati inayozalishwa kupitia jua pamoja na ile inayotokana na maji, hii ikionesha nia ya China ya kufadhili nishati inayoweza kutumika tena badala ya nishati ya makaa ya mawe.

Bado, takwimu za mwaka jana hazijatoa mwelekeo wazi wa ushirikiano wa kifedha wa China na Afrika, kwasababu taasisi za China pia zilitoa mikopo kwa mataifa yalio na uchumi uliodorora kama Nigeria na Angola.

Kituo hicho cha utafiti kimesema kinasubiri kuona iwapo ushirikiano wa China na mataifa ya Afrika utadumisha ubora wake.