China na Brazil zakubaliana kuimarisha uhusiano
14 Aprili 2023Rais wa China Xi Jinping amemueleza mwenzake wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva kwamba maendeleo ya China yatafungua fursa mpya kwa Brazil na ulimwengu mzima na kwamba wanapaswa kuimarisha ushirikiano pamoja na uwezo wao katika sekta mbalimbali kuanzia kilimo hadi miundombinu.
Mazungumzo yao yamefanyika katika siku ya pili ya ziara ya kikazi ya Lula nchini China, ambalo ni taifa mshirika mkubwa na muhimu si tu wa kibiashara bali pia katika jaribio la Brazil la kutoa upinzani dhidi ya taasisi za magharibi ambazo kwa muda mrefu zina ushawishi mkubwa katika eneo la kiuchumi kimataifa.
Mazungumzo yao yalijikita kwa kiasi kikubwa katika ushirikiano wa kibiashara lakini pia aina nyingine za ushirikiano. Aidha wakuu hao walijadiliana kuhusu mzozo wa Ukraine na kukubaliana juu ya umuhimu wa kuumaliza mzozo huo kwa njia ya makubaliano.
"Nina hakika kwamba maendeleo endelevu na uhusiano thabiti kati ya China na Brazil yatatoa fursa chanya na muhimu katika kukuza amani, utulivu, ustawi na maendeleo ya kikanda na kwingineko," alisema Xi.
Xi na Lula aidha walishuhudia tukio la kutiliana saini makubaliano yanayogusa sekta kadha wa kadha kuanzia kilimo hadi teknolojia ya angani, hali inayodhihirisha kuimarika kwa mahusiano yaliyogubikwa na mivutano ya kila wakati, chini ya utawala wa mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia Jair Bolsonaro.
Katika hatua nyingine China kwa mara nyingine, imezuia uingiliaji wowote wa kigeni linapokuja suala la Taiwan, baada ya mazungumzo kati ya waziri wa mambo ya nje Qing Gang na mwenzake wa Ujerumani Annalena Baerbock aliyeko ziarani China.
Baerbock awali alielezea wasiwasi wake juu ya mvutano ulioko kuelekea kisiwa hicho na kuonya hatua yoyote ya kuvuruga utulivu wake itakuwa na athari kubwa akiangazia hasa asilimia 50 ya biashara ulimwenguni inayotumia ujia wa Bahari wa Taiwan.
Wasiwasi umeongezeka na hasa baada ya Urusi kuivamia Ukraine kwamba huenda China ikachukua msimamo kama huo dhidi ya Taiwan na mzozo kuwa mkubwa zaidi, ukiihusisha pia Marekani inayopingana na China. Mashaka hayo yanaongezwa chumvi na hatua ya Beijing ya kukataa kulaani uvamizi wa Urusi.
Soma Zaidi: Macron azuru China kuishinikiza kusaidia amani nchini Ukraine