1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Rais wa Brazil kuizuru China

12 Aprili 2023

Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva ameelekea China kwa ziara rasmi yenye lengo la kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili, ambapo pia anatarajiwa kuzungumzia pia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4Pwf9
Luiz Inacio Lula da Silva - 100 Tage als Präsident im Amt
Picha: Eraldo Peres/AP/picture alliance

Lula ambaye aliondoka siku ya Jumanne, anatarajiwa kuwasili Jumatano mjini Shanghai, amepangiwa kukutana na Rais Xi Jinping mjini Beijing siku ya Ijumaa. China ambalo ni taifa kubwa barani Asia pamoja na Brazil, yenye uchumi mkubwa katika eneo la Amerika Kusini, zote ni wanachama wa kundi la nchi zilizoendelea na zinazoinukia kiuchumi, G20. China ni mshirika muhimu zaidi wa kibiashara wa Brazil, na pia ni moja kati ya vyanzo muhimu zaidi vya uwekezaji wa kigeni.

Ziara ya Lula kuimarisha uhusiano wa kirafiki

Ziara ya Lula nchini China iliyoahirishwa mwezi Machi kutokana na sababu za kiafya, inalenga kuimarisha tena uhusiano na China baada ya uhusiano huo kudorora kwa kipindi cha miaka minne wakati wa mtangulizi wake mwenye kufuata siasa kali za mrengo wa kulia, Jair Bolsonaro.

Akizungumza Jumanne na waandishi habari, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin amesema ziara ya Rais Lula itakayofanyika kuanzia Aprili 12 hadi 15, itaimarisha uhusiano wao wa kirafiki katika nyanja mbalimbali.

''China inapenda na iko tayari kufanya kazi na Brazil, na tunaichukulia ziara hii kama fursa ya kuimarisha ushirikiano wetu, kusisitiza mazingira mazuri katika kukuza mshikamano na uratibu miongoni mwa nchi zinazoendelea, na kushughulikia kwa pamoja changamoto za ulimwengu,'' alisema Wenbin.

China Frankreich Emmanuel Macron Xi Jinping
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron na Rais wa China, Xi JinpingPicha: Ng Han Guan/AP/picture alliance

Aidha, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine pia utakuwa miongoni mwa ajenda katika ziara ya Lula. Wiki iliyopita, Lula aliwaambia waandishi habari kwamba atakapokutana na Xi, atapendekeza mpango wa upatanishi wa kimataifa wa amani kati ya Urusi na Ukraine, juhudi ambazo zimepongezwa tu na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, miongoni mwa viongozi wa mataifa ya Magharibi.

''Nina uhakika kwamba Ukraine na Urusi zinasubiri mtu mwingine aseme kitu. Tukae chini na tuzungumze,'' alisisitiza rais huyo wa Brazil Lula aliyeingia madarakani Januari Mosi, amependekeza kuwa suluhisho la amani linaweza kurejeshwa kwa eneo jipya lililovamiwa, ingawa sio Rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Urusi mwaka 2014, mpango ambao Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameukataa moja kwa moja.

Brazil inaitegemea China

Mwanadiplomasia mmoja wa Umoja wa Ulaya mjini Brasilia amesema ili juhudi zake ziweze kuendelea, Lula anaihitaji China kupeleka ujumbe kwa Urusi. Amesema Lula anafahamu vizuri kuwa China ndiyo nchi pekee ambayo Urusi itaisikiliza.

Katika ziara hiyo, Lula anaongozana na ujumbe wa mawaziri wanane na magava wa majimbo saba ya kaskazini mashariki mwa Brazil. Takribani mikataba 20 itasainiwa, ikiwemo kuundwa kwa satelaiti ya sita ya mpango wa pamoja ulioanzishwa mwaka 1988, ambayo itatumika kuufuatilia Msitu wa Amazon.

Wakati huo huo, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock wanatarajiwa kuizuru China kuanzia Aprili 13 hadi 15. Taarifa iliyotolewa Jumatano na wizara ya mambo ya nje ya China, imeeleza kuwa China na Ujerumani zitafanya mazungumzo ya kimkakati ya kidiplomasia na usalama.

(DPA, AFP, Reuters)