Chanjo za ugonjwa wa Mpox zaanza kutolewa Afrika
20 Septemba 2024Kulingana na kituo cha CDCdozi 300 za kwanza zilitolewa mnamo siku ya Jumanne karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Nchi hiyo ndio imeathirika zaidi, ikiwa na takribani visa 24,000 na zaidi ya vifo 700 vinavyohusishwa na kirusi cha Mpox kati ya Januari na Agosti.
Akizungumza kwa njia ya simu na waandishi wa habari, mkurugenzi wa CDC Jean Kaseya amesema zoezi la chanjo nchini Kongo litaanza katika wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba. Lakini amethibitisha kwamba Rwanda imeanza zoezi hilo tangu Septemba 17na kuzilenga wilaya 7 zinazopakana na Kongo.
"Chanjo ambayo Rwanda inatumia, na niliambiwa kwamba walianza siku mbili zilizopita, tayari wamewachanja karibu watu 500. Walipata dozi 1,000 na wanahitaji zaidi ya kile walichoomba, dozi 10,000."
Na mamlaka nchini Kongo zinasema zoezi la utoaji chanjo litaanza Oktoba 2 huku nchi hiyo ikirekodi zaidi ya visa 24,000. Kampeni ya chanjo nchini humo itadumu kwa siku 10, kwa mujibu wa Daktari anayeongoza kitengo cha kukabiliana na Mpox Adelard Lofungola.
Soma:Rwanda yaanza zoezi la kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa mpox
Mtaalamu huyo aliwaeleza waandishi wa habari mjini Kinshasa kwamba wataanza na wahudumu wa afya, watoto na makundi muhimu kama vile wafanyakazi wanaojihusisha na biashara ya ngono. Kongo hadi sasa imepokea dozi 265,000zilizotolewa na Umoja wa Ulaya na Marekani ambazo zimezalishwa na kampuni ya Denmark ya Bavarian Nordic.
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus ameonya kwamba sio tu wanakabiliana na mlipuko mmoja bali ni milipuko "kadhaa" katika maeneo tofauti inayosababishwa na aina tofauti ya virusi hasa akiangazia hali ya Burundi na Kongo "ambapo visa vinaendelea kuongezeka".
Kulingana na vigezo vya awali vya WHO, chanjo ya Mpox inaweza kutolewa kwa watu walio na umri wa zaidi ya miaka 18 ambapo dozi mbili zitatolewa kwa kipindi cha wiki nne tofauti. Lakini kutokana na visa vingi na vifo kuripotiwa miongoni mwa watoto nchini Kongo, WHO imesisitiza kwamba chanjo ya Mpox inaweza kutumika katika hali isiyo ya kawaida kwa watoto, vijana, wanawake wajawazito na watu walio na upungufu wa kinga.Visa vya Mpox vyafikia 25 nchini Afrika Kusini
Shirika hilo hata hivyo linasisitiza kwamba kunahitajika data zaidi kuhusu usalama na ufanisi wa chanjo katika hali kama hizo. Data zilizopo kwa sasa zinaonyesha kuwa dozi moja ya chanjo ya MVA-BN inayotolewa kabla ya kuambukizwa inakadiriwa kuwa na ufanisi wa asilimia 76 katika kinga dhidi ya Mpox huku dozi mbili zikiwa na ufanisi wa hadi asilimia 82.