Afrika CDC: Magharibi hawapaswi kuitelekeza Afrika mpox
13 Septemba 2024Mkuu wa Taasisi ya kuzuwia na kupambana na magonjwa ya Umoja wa Afrika amesema ni wakati kwa nchi za Magharibi kuonyesha kuwa zimejifunza kutokana na janga la Uviko-19 na sio kuitelekeza Afrika wakati wa mlipuko wa homa ya nyani.
Ugonjwa huo unaoitwa mpox ulitangazwa na shirika la afya duniani kuwa dharura ya kimataifa, kufuatia ongezeko la visa vya aina mpya ya kirusi chake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo ndiyo kitovu cha mlipuko huo.
Kituo cha kuzuwia na kupambana na magonjwa cha Umoja wa Afrika -Africa CDC, kimesema kina pungufu ya dola milioni 600 kinazohitaji kukabiliana na ugonjwa huo ambao hivi sasa umesambaa katika mataifa 14 barani Afrika.
Wakati wa mshikamano
Hata hivyo mkuu wa Africa CDC Jean Kaseya amesema ana matumaini lengo la ufadhili litafikiwa, kwa sababu ni wakati kwa mataifa ya magharibi kuonyesha kuwa yalijifunza kutokana na janga la Uviko.
"Hatutaki kurudi tena kesho kusema, mmeitelekeza tena Afrika," alisema wakati wa mkutano wa mtandaoni kuhusu mpox.
"Tunataka waelewe somo hili kusema ni wakati wao wa kujenga upya uaminifu."
Soma pia: Ugonjwa wa mpox watangazwa kuwa dharura ya afya ya umma
Ukosoaji ulielekezwa kwa mataifa ya Magharibi wakati wa janga la Covid-19, kwa madai kwamba waliitupa mkono Afrika kwa kuhodhi chanjo au kwa kuweka kipaumbele kwa mataifa tajiri.
"Kama tunavyojua, uaminifu ulivunjika kati ya nchi za Magharibi na Afrika. Ni wakati wa mshikamano," alisema Kaseya.
Kulingana na takwimu za hivi karibuni za Taasisi ya Afya ya Umma ya Kongo, kumekuwa na karibu visa 22,000 na vifo 716 vilivyohusishwa na virusi vilivyorekodiwa tangu Januari.
Kaseya pia alionya kwamba kiwango cha upimaji kimesalia kuwa "suala kuu", akisema uwezo wa upimaji unahitajika kuongezwa ili kuufuatilia vyema mlipuko huo.
Hadi sasa, karibu dozi 200,000 za chanjo zimewasilishwa DRC na Umoja wa Ulaya, pamoja na nyingine takriban 50,000 kutoka Marekani.