1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Mpox yatangazwa kuwa dharura ya afya ya umma

14 Agosti 2024

Kituo cha kudhibiti na kuzuwia magongwa barani Afrika, Africa CDC, kimeutangaza mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nyani, au mpox ulioathiri nchi kadhaa zaAfrika hasa nchini Kongo, kuwa dharura ya afya ya umma.

https://p.dw.com/p/4jRqe
Congo Mpox
Ugonjwa wa mpox watangazwa kuwa dharura ya afya ya ummaPicha: AP/picture alliance

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) kilitangaza kwa mara ya kwanza hali ya dharura ya kiafya barani Afrika huku, mkutano wa dharura wa shirika la afya duniani, WHO unajitayarisha kuamua iwapo itangaze dharura ya kimataifa kuhusiana na mlipuko huo.

Wataalam wanatumai mikutano hii itachochea hatua za kimataifa, ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto ya upatikanaji mdogo wa chanjo, ufadhili na uwepo wa milipuko mingine ya magonjwa.

Africa CDC yatangaza dharura ya kiafya kutokana na homa ya nyani Afrika

Mjini Goma, mvutano unazidi kuongezeka huku taarifa za mlipuko wa mpox zikienea. Mji huu, ambao tayari umedhoofishwa na migogoro ya kivita, sasa unakabiliwa na tishio jipya la kiafya. 

Visa vya mpox vilivyogunduliwa hapa vinashughulikiwa katika vituo vya afya vya mji huo. Lakini wengi wanalalamika kwamba hawajapewa taarifa za kutosha kuhusu ugonjwa huo.

“Mara tu walipotangaza mpox kuwa hali ya dharura ya kiafya, nilianza kujiuliza maswali, sisi hapa Goma, tutafanya nini? Hakuna chanjo, hatujui tufanye nini, hatujui ni hatua gani za kujikinga, imekuwa hali mbaya. Nimeanza kuwa na hofu, hasa na familia ambazo ziko hapa Goma. Hali hapa mashariki ni ngumu, kuna wakimbizi wengi ambao hawajui namna ya kupata huduma za afya, hatuelekezwi kuhusu hatua za kujikinga, hakuna tahadhari,” alisema mmoja ya raia wa Goma ambae hakutaka jina lake litajwe.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndio iliathirika zaidi na Mpox

Homa ya Nyani
Rais wa Kongo wasema hawajapewa taarifa ya kutosha kuhusu homa ya nyani Picha: Arlette Bashizi /REUTERS

Kumekuwa na zaidi ya visa 15,000 vinavyoshukiwa kuwa vya mpox barani Afrika mwaka huu na vifo 461, hasa miongoni mwa watoto humu nchini DRC, kulingana na kituo cha Africa CDC. 

Maambukizi ya virusi kawaida huwa madogo lakini yanaweza kusababisha kifo, na husababisha dalili zinazofanana na mafua na vidonda vilivyojaa usaha.

Aina mpya ya virusi imesababisha milipuko katika kambi za wakimbizi mashariki mwa DRC mwaka huu, na kuenea kwa mara ya kwanza nchini Uganda, Burundi, Rwanda, na Kenya.

Maafisa wa Afya wahofia mlipuko wa homa ya nyani kote barani Afrika

Trésor Hamiri Hemedi, daktari na mtaalamu wa afya ya umma DRC, anadhani suluhu la kukabiliana na hali hii ni uhamasishaji.

“Katika hali kama hizi za dharura, kinachoweza kushauriwa ni kubaki mtulivu na kuwa na subira, huku tukijua kwamba serikali iko hapa kutafuta hatua za kinga. Ni muhimu kuwa na uhamasishaji mzuri, na mawasiliano mazuri ndani ya jamii ili hatua za kinga zichukuliwe na kuzingatiwa na umma ili kuepuka kuenea kwa maambukizi.”

Wataalamu humu nchini waliruhusu matumizi ya chanjo katika ngazi ya kitaifa mnamo Juni, lakini serikali bado haijaomba rasmi dozi yoyote kutoka kwa watengenezaji, wala kutoka kwa serikali kama vile Marekani inayotaka kutoa msaada kupitia muungano wa kimataifa wa chanjo, Gavi.

Mwandishi: Ruth Alonga