'Burundi iwaachie huru watetezi wa haki za binaadamu'
14 Machi 2023Mashirika hayo ya haki za binaadamu aidha yamezitaka mamlaka hizo kufuta madai yasiyo na msingi dhidi ya wanaharakati hao.
Kulingana na mashirika hayo ya kimataifa ya Amnesty International na Human Rights Watch pamoja na utetezi wa haki za binaadamu la nchini Burundi, la Burundi Human Rights Initiative, watetezi hao wanatuhumiwa kwa uasi na kudhoofisha usalama wa ndani wa serikali. Madai hayo ni kama yanahusishwa na mashirikiano baina ya watetezi hao na shirika la kimataifa la nje ya nchini pamoja na ufadhili walioupokea kutoka kwa shirika hilo.
Watetezi wawili miongoni mwao wanafanya kazi na Muungano wa mashirika ya mawakili wanawake nchini Burundi, AFJB na watatu wengine kutoka Muungano wa Amani na utetezi wa Haki za Binaadamunchini humo, APDH.
Februari 16, waziri wa mambo ya ndani, maendeleo ya jamii na usalama wa umma wa Burundi Martin Niteretse aliyashutumu mashirika hayo kwa kushirikiana na shirika moja la kimataifa lisilo la kiserikalim hatua iliyopelekea wanaharakati wanne kukamatwa ambao ni rais wa AFJB, Sonia Ndikumasabo na mratibu mkuu wa muungano huo Marie Emerusabe. Wengine waliokamatwa ni mwakilishi wa kisheria wa APDH Audace Havyarimana na mkurugenzi mtendaji Sylvana Inamahoro ambao walizuiwa makao makuu ya Idara ya Ujasusi nchini Burundi, SNR na baadae kuhamishiwa katika gereza ya Mpimba.
Niteretse ameviambia vyombo vya habari kwamba kesi dhidi ya wanaharakati hao inaendelea na kuongeza kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba huenda wangetumia fedha walizopewa kwa kufadhili ugaidi. Akasema ni muhimu kuwa waangalifu kwa kila jambo ili kuhakikisha hakuna chochote kinachovuruga amani na utulivu wa umma.
Mashirika hayo mawili yanajishughulisha na kupambana na unyanyasaji wa kijinsia na haki za ardhi yamesajiliwa nchini Burundi na husaidia makundi yaliyotengwa zaidi nchini humo na hatua ya serikali ya kuwafungulia mashtaka watetezi hao imezusha hofu ya kutokea msako mwingine wa mashirika ya kiraia nchini Burundi na kudhoofisha ajenda ya rais juu ya mageuzi, yamesema mashirika hayo.
Oktoba 2018, mamlaka zilisimamisha shughuli za mashirika mengi ya nje nchini Burundi na kuyalazimisha kusajiliwa, hatua iliyowataka pia kuwasilisha taarifa zinazoonyesha makabila ya waajiriwa wao. Sera hiyo ya serikali, iliyozingatia sheria ya mashirika ya kigeni yasiyo ya kiserikali, na kupitishwa Januari 2017 iliyafanya mashirika mengi kufunga shughuli zao kutokana na hofu kwamba wafanyakazi wao watalengwa kwa misingi ya ukabila.
Carina Tersakian kutoka Shirika la Haki za Kibinadamu la Burundi, amesema madai dhidi ya wanaharakati hao yanayohatarisha usalama wa taifa na uasi dhidi ya watetezi wa haki za binadamu ni ya kipuuzi. Akaongeza kuwa iwapo mamlaka zina maswali kuhusu vyanzo vyao vya ufadhili wao, basi yangeweza kutatuliwa kupitia njia za kawaida za kiutawala, kama ilivyoainishwa kwenye sheria.
Tangu Rais Évariste Ndayishimiye aingie madarakani Juni 2020 na kutoa ahadi za kurejesha uhuru wa kujieleza na kujumuika, lakini uadui kati ya serikali na jumuiya ya kiraia na vyombo vya habari vya Burundi uko palepale. Naibu mkurugenzi wa Kanda wa shirika la Amnesty international Flavia Mwangovya amesema matendo yana nguvu kubwa zaidi ya maneno na iwapo mamlaka zinataka kutimiza ahadi yao juu ya haki za binaadamu zinalazimika kuruhusu mashirika ya kiraia kufanya shughuli zao ambazo ni pamoja na kutetea na kuwasaidia wahanga wa ukiukwaji wa haki za binaadamu.
Soma Zaidi: Rais Ndayishimiye azungumzia utawala bora Burundi