1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Evariste awakemea waharibifu wa usalama Burundi

26 Mei 2021

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amesema amekasirishwa na makundi ya watu walio na nia ya kuiharibia nchi kupitia vitendo vya ugaidi. Hii ni baada ya mashambulizi ya guruneti katika maeneo matatu mjini Bujumbura

https://p.dw.com/p/3tzw8
Burundi Gitega | Beerdigung des ehemaligen Präsidenten Pierre Nkurunziza: Evariste Ndayishimiye hält Ansprache
Picha: Getty Images/AFP/T. Nitanga

Tamko la polisi ya taifa limesema watu wawili walipoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mashambulizi ya guruneti kwenye maeneo matatu ya mji mkuu Bujumbura.

Guruneti la kwanza iliripuliwa kwenye eneo la kibiashara la Plaza kando mwa soko kuu la zamani la Bujumbura, na lingine katika kituo cha mabasi ya uchukuzi wa abiria na vitu huku guruneti la 3 likiripuliwa eneo linalotambulika kama Permenance pia kwenye kituo cha mabasi.

Mashambulizi hayo yalisababisha hali ya taharuki kwani yalitokea majira ya saa moja usiku wakati raia wengi wakielekea kwenye mabasi kwa usafiri baada ya siku nzima ya kazi. Bado polisi haijatoa maelezo zaidi juu ya mashambulio hayo huku kwenye mitandao ya kijamii zikizagaa picha za wahanga wa mashambulizi hayo.

Baadhi ya raia wameiambia DW,  wamesikitishwa na hali hiyo waliyoitaja kama ya kuja kuirudisha Burundi nyuma. Raia wameitaka serikali kuhakikisha wahusika wamekabiliwa na mkono wa sheria.

Polisi waimarisha usalama mjini Bujumbura

Burundi Polizei Sicherheitskräfte Militär Symbolbild
Polisi wakishika doria mjini Bujumbura, Burundi Picha: picture-alliance/AA/N. Renovat

Hali kwa sasa imeonekana kurejea kuwa ya kawaida huku askari polisi wakionekeana kwa wingi katika maeneo tafauti ya mji mkuu.

Kupitia anuani yake ya Twita rais Evariste Ndayishimiye amelaani mashambulizi hayo na kusema amekasirikishwa kuona bado kuna makundi ya watu ambao nia yao ni kuiharibu Burundi kupitia vitendo vya ugaidi. Rais Ndayishimiye ametowa salamu za rambi rambi kwa familia  zilizopoteza watu wao katika mashambulizi hayo na kuwataka raia kuimarisha utangamano.

soma zaidi: Watu 8 wauwawa katika shambulizi Burundi

Risala kama hiyo imetolewa pia na mpatanishi wa kitaifa Edouard Nduwimana, ambaye mbali na kulaani mashambulizi hayo amesema yamekuja wakati Burundi ikipokea kikao cha 51 cha kamati ya Umoja wa mataifa, inayoangazia maswala ya usalama katika nchi za kati mwa Afrika.

Mashambulizi hayo yametokea wakati Mkutano wa umoja wa Ulaya unatarajiwa kutoa uamuzi wa kusitisha au kutositisha vikwazo uliyoiwekea Burundi tangu 2015.

Mwandishi: Amida Issa DW, Bujumbura